RUFAA ya kesi ya mauaji iliyomkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam (RCO), Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe na wenzake watatu imeanza kusikilizwa jana katika Mahakama ya Rufani huku pande zote mbili zikiwasilisha hoja zake.
Kusikilizwa kwa rufaa hiyo kumetokana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kupinga uamuzi uliotolewa Agosti 17, 2009 katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam uliowaacha huru watu wanne akiwemo Zombe na wenzake waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji.
Kuachiwa huko kulitokana na maelezo kuwa upande wa Jamhuri ulishindwa kupeleka ushahidi mzuri ambao ungeweza kuishawishi mahakama hiyo iwaone washtakiwa hao wana hatia.
Wakibishana kwa hoja katika mahakama hiyo iliyopo Dar es Salaam mbele ya Jaji Benard Luanda wakati upande wa mawakili wa Serikali uliongozwa na Timothy Vitavi, aliyedai kuwa wanapinga kuachiwa huru kwa watuhumiwa hao kwa kuwa ushahidi uliotolewa katika kesi ya msingi ulikuwa hauna shaka.
“Kimsingi washtakiwa wote walikuwa na kosa la mauaji kwa kuwa upande wetu hoja zimewasilishwa zilikuwa hazina tatizo,” alidai Vitavi.
Alidai watazidi kupinga kuachiwa kwao kwa kuwa ushahidi wa awali ulikuwa hauna shaka dhidi ya kosa lililokuwa likiwakabili.
Kwa upande wa utetezi ulioongozwa na Wakili Richard Rweyongeza, ulipinga na kudai kuwa wateja wao hawana makosa na wala hawakushiriki katika tukio hilo la mauaji hivyo waliitaka mahakama hiyo itende haki.
Akiendelea kutoa hoja zake, Rweyongeza ambaye ni Wakili wa Zombe, alidai kuwa katika tukio hilo mteja wake hakufanya kitendo hicho.
“Wanaotuhumiwa walitajwa tu na kesi nyingi huwa watu wanasingiziwa sasa kwa hapa ilipofikia tunaomba mahakama iangalie suala hili kwa kuwa kesi iliisha na sijaelewa kwanini jalada limerudishwa tena,” alidai Rweyongeza.
Baada ya kusikiliza pande zote mbili, mahakama hiyo ilisema ipewe muda ili msajili aweze kupitia hoja hizo kisha atangaze tarehe kwa ajili ya kusoma hukumu.
Hata hivyo, Jaji Luanda, aliagiza kuwa hoja zote ni za msingi hivyo ziwasilishwe kwa Msajili wa Mahakama Kanda ya Dar es Salaam kwa ajili ya kutolea majibu yatakayoelekeza kuendelea kusikilizwa ama la.
Zombe na wenzake walidaiwa kuwa Januari 14, 2006 waliwaua wafanyabiashara watatu wa madini wa Ulanga mkoani Morogoro ambao ni Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi na Mathias Lukombe pamoja na dereva teksi Juma Ndugu, mkazi wa Dar es Salaam kwa madai kuwa walikuwa majambazi.
Post a Comment