HEDHI ni mzunguko wa kila mwezi ambao huleta kutokwa na damu ukeni
kutokana na mimba kutotungwa. Kwa kawaida hedhi ya kwanza hutokea katika
umri wa miaka 12 -13. Mzunguko huu wa hedhi huwa unadhibitiwa na
homoni zinazozalishwa na mwili.
Hedhi hutokea pale ambapo tishu za ukuta wa mji wa mimba unabomoka na kutoka kama damu ukeni.
Kila mwezi ovari za mwanamke huzalisha yai moja la uzazi. Yai hili
huweza kukaa kwa muda mpaka wa saa 36 ndani ya mirija na tumbo la uzazi.
Inapotokea yai hili halijarutubiwa, ukuta wa mji wa uzazi hubomoka na
kutoka kwa njia ya uke pamoja na damu. Hali hii huitwa hedhi.
Mzunguko wa hedhi huanza kuhesabiwa siku ya kwanza mwanamke anapoanza kupata siku zake.
Sasa basi, mwanamke anapoingia katika mzunguko huo anapaswa kuwa makini ili kuboresha afya yake.
Kwa sababu hiyo, mtandao wa asasi za kiraia wa Tanzania Water and
Sanitation Network (TAWASANET) umeamua kutoa elimu shuleni kwa walimu na
wanafunzi wa kike juu ya namna ya kujisitiri wakati wa hedhi.
Lengo ni kuhakikisha kwamba kadiri muda unavyosonga mbele huduma ya
kujisitiri katika kipindi cha hedhi hasa kwa wasichana walioko shuleni
inaangaliwa kwa ukaribu zaidi.
Mratibu wa TAWASANET, Emmanuel Jackson, anasema hedhi katika Bara la
Afrika inachukuliwa kama jambo la siri na la aibu kabisa ambalo
haliwezi kuzungumzwa na watu wala kulisema hadharani, katika mfumo huu
jamii imekuzwa kiasi kwamba haiwezi tena kushughulikia changamoto
zinazohusiana na hethi.
Jackson anasema ugumu wa kushindwa kushughulikia changamoto za hedhi
kunawaathiri zaidi wasichana walioko shuleni, hii ni kwa sababu
changamoto hizo zinagusa kwa namna moja ama nyingine mfumo wa kujifunza
unaochangiwa na mazingira pamoja na miundombinu ya shuleni na mifumo
iliyopo majumbani.
“Ili wanafunzi wa kike wawe na afya bora, shule zinapaswa kuwa na
vyoo rafiki kwa wasichana, sehemu ya kubadilishia na kutunzia
vihifadhio, (mfano pedi) maji safi, utaratibu mzuri wa usafi
ikujumuisha unawaji mikono kwa sabuni, pamoja na ukaribu na walimu.
“Pasipo upatikanaji wa vifaa hivi ikijumuisha na mazingira rafiki
kwa wasichana, ufaulu wa wasichana unabaki kuwa shakani,” anasema
Jackson.
Huduma ya kujisitiri na ufaulu
Dk. Hamis Malebo, kutoka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya
Binadamu (NIMR), anasema mfumo mzuri wa kiafya shuleni ni ule ambao
desturi na taratibu zinaandaliwa na kusimamiwa kwa kuliona suala la
hedhi kuwa ni la aibu, matokeo yake msichana hapati ushirikiano wa
kutosha katika mazingira ya nyumbani, shuleni na kwa jamii inayozunguka.
Anasema hii inamaanisha kwamba msichana anaachwa apambane na
changamoto hizo peke yake hata kama hana uwezo kwa wakati huo kimwili,
kiakili, kisaikolojia au hata kifedha.
Dk. Malebo anasema katika mfumo wa elimu wa sasa kwa maeneo mengi
nchini, wasichana wanakabiliwa na gharama kubwa za kununua vihifadhio
mfano pedi.
“Hii inasababisha wasichana kuchagua njia rahisi ambazo haziwahifadhi
kwa ufanisi ama kutafuta njia mbadala (mfano kuwa na uhusiano na
wanaume) ili wapate fedha za kutimiza mahitaji ikiwemo vihifadhio.
“Upungufu wa maji kwa ajili ya kuoga ama kujisafisha wakati wa
kipindi cha hedhi, au kusafisha vihifadhio(kwa wanaotumia njia ya asili)
hali hii inaongeza hofu kwa wasichana kuhisi kuwa watatoa harufu
mbaya, ama kuwa na hisia kuwa hawako safi wanapokuwa kati ya wanafunzi
wengine,” anasema Dk. Malebo.
Anasema uchafu wa vyoo ama visivyofaa kwa matumizi hasa kwa wasichana wanaoingia katika hedhi, huleta changamoto kubwa kwao.
Anasema kuvuja kwa hedhi kutokana na kutumia vihifadhio vilivyo
katika viwango vya chini ni kitendo ambacho huwadhalilisha wasichana.
Dk. Malebo anasema kutokuwa na walimu wanaotoa msaada stahiki kwa
wasichana walio katika hedhi mfano kuwapa ruhusa kwenda chooni au chumba
cha kubadilishia wakati vipindi vya darasa vikiendelea ama kutokuwa na
adhabu kali zinazoweza kuongeza uwezekano wa kudhalilika.
Anasema kutokana na msongo wa kuhisi aibu changamoto hizi husababisha
wasichana shuleni kuchagua kubaki nyumbani na kutohudhuria masomo
katika kipindi cha hedhi na wengine wameripotiwa kuacha kabisa masomo.
Inasemekana kuwa baadhi ya wasichana hukosa masomo kati ya siku moja
hadi saba ama zaidi katika kipindi cha kila mwezi ambapo sababu kubwa
zinazochangia ni pamoja na hofu ya kushindwa kudhibiti hedhi (kuvuja)
hatimaye kudhalilika akiwa shuleni hasa anapotakiwa na mwalimu kuandika
ubaoni akiwa na wenzake darasani.
“Wapo wengine ambao hukabiliwa na maumivu makali hasa katika siku
mbili za awali hivyo hupungukiwa na uwezo wa kufuatilia masomo na
wengine huwa na hali ya kutojisikia vizuri hatimaye kushindwa kuhudhuria
masomo.
“Wengine hufanya siri hivyo njia rahisi inayochaguliwa ni kutofika shuleni ili wawe salama,” anasema Dk. Malebo.
Hali halisi ya mazingira ya shule
Mhandisi kutoka taasisi ya Water Supply and Sanitation Collaboretive
Council (WSSCC) Wilhemina Malima anasema programu za elimu, ikijumuisha
kwa shule za msingi na sekondari, zimeboresha kuongezeka kwa udahili wa
wanafunzi shuleni.
Anasema
hata hivyo, uwiano hauko sawa baina ya udahili na uboreshaji wa
miundombinu itakayokuwa rafiki hasa kwa wasichana wanapokuwa katika
kipindi cha hedhi.
Nini kifanyike?
Ili kuweka mazingira mazuri zaidi ya ufaulu kwa wasichana walio shuleni, ni muhimu wanafunzi wawe na uhakika wa kupata pedi.
Hii inatokana na uhalisia wa hali duni ya kiuchumi wanayokabiliana
nayo baadhi yao ambapo hushindwa kununua vihifadhio hatimaye kutafuta
njia mbadala, endapo kama kutahitajika kuchangia uandaliwe utaratibu
mzuri, mfano kwa wazazi au kwa wanajamii badala ya kuchangisha
wasichana ambao hawana vyanzo vya mapato.
Pia Serikali inashauriwa kuidhimisha sehemu ya fedha ya
ruzuku(Capitation Grant) kuchangia upatikanaji wa pedi, pia shule ziweke
mipango ya upatikanaji wa fedha kwa ajili hiyo.
Pia elimu ya afya ya uzazi itolewe kwa wasichana ili waweze
kujitambua na kujihifadhi vizuri hasa wanapokuwa katika kipindi cha
hedhi, kwa waalimu ili kuongeza ujuzi namna ya kuwasaidia wasichana,
kwa jamii ili waondokane na mila na desturi zinazowaathiri watoto.