Mheshimiwa Spika, hali ya uchumi inatathminiwa pia kwa kuangalia mwenendo wa biashara ya nje na akiba ya fedha za kigeni. Katika
mwaka 2016, nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamishaji
mali nchi za nje (current account deficit) ilipungua kwa asilimia 48.8
na kufikia nakisi ya Dola za Kimarekani milioni 2,054.8, kutoka nakisi
ya Dola za Kimarekani milioni 4,011.6 kwa mwaka 2015. Kupungua huko
kulitokana zaidi na ongezeko la thamani ya madini hususan dhahabu,
bidhaa asilia, mapato yatokanayo na utalii, pamoja na kupungua kwa
thamani ya bidhaa zilizoagizwa kutoka nje ya nchi hususan bidhaa za
kukuza mitaji, na bidhaa za matumizi ya kawaida. Katika kipindi hicho,
thamani ya bidhaa na huduma zilizouzwa nje ya nchi ziliongezeka kwa
asilimia 5.2 na kufikia Dola za Kimarekani milioni 9,381.6 wakati
thamani ya bidhaa na huduma toka nje zilipungua kwa asilimia 13.7 na
kufikia Dola za Kimarekani milioni 10,797.4
Mheshimiwa Spika, hadi mwezi
Desemba 2016, akiba ya fedha za kigeni ilifikia Dola ya Kimarekani
milioni 4,325.6 ambazo zinatosheleza kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje
ya nchi kwa takriban miezi 4.2. Aidha, rasilimali za fedha za kigeni za
mabenki ya biashara zilifikia Dola ya Kimarekani milioni 768.2, wakati
amana za fedha za kigeni zilizohifadhiwa na wakazi katika benki za
biashara zilifikia Dola za Kimarekani milioni 2,870.8. Hivyo, akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kuridhisha.
Mwenendo wa Sekta ya Kibenki
Mheshimiwa Spika, kiashiria kingine cha hali ya uchumi ni mwenendo wa sekta ya fedha. Katika
kipindi kilichoishia Desemba 2016, tathmini ya hali ya mabenki yetu na
taasisi za fedha inaonesha kuwa mabenki yetu ni imara na salama, yakiwa
na mitaji na ukwasi wa kutosha: Kiwango cha mitaji kikilinganishwa na
mali iliyowekezwa (total capital to total risk weighted assets and
off-balance sheet exposures) kilikuwa asilimia 17.8 kikilinganishwa na
kiwango cha chini kinachotakiwa kisheria cha asilimia 10.0.
Hali ya Ukwasi katika uchumi
Mheshimiwa Spika, ukwasi
(liqudity) ni kiasi cha fedha kilichopo katika uchumi na unajumuisha
fedha taslim, amana katika mabenki zilizopo Benki Kuu. Utoshelevu wa
ukwasi katika uchumi unapimwa kwa kuangalia viashiria mbalimbali ikiwemo
ujazi wa fedha, mwenendo wa mikopo kwa sekta binafsi, kiwango cha
mitaji ya mabenki, uwiano kati ya mali inayoweza kubadilishwa kuwa fedha
taslim na amana zinazoweza kuhitajika katika muda mfupi, na upatikanaji
wa huduma za kifedha. Pale ambapo imedhihirika kuwa kuna upungufu wa
ukwasi katika uchumi, Serikali kupitia Benki Kuu huchukua hatua
mbalimbali za kisera kuchochea shughuli za kiuchumi. Hatua hizi ni
pamoja na kuongeza ujazi wa fedha na kuboresha mazingira kwa sekta
binafsi kukopa. Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango
inaweza kupunguza kodi na kuongeza matumizi ya Serikali.
Hali ilivyo sasa
Mheshimiwa Spika,
hali ya baadhi ya vigezo vya ukwasi nchini ni kama ifuatavyo: kwa
kutumia kigezo cha uwiano kati ya mali inayoweza kubadilishwa kuwa fedha
taslim na amana zinazoweza kuhitajika kwa muda mfupi (Liquid assets to
Demand Liabilities), uwiano
huu ulikuwa asilimia 42.4 ukilinganishwa na asilimia 37.2 katika
kipindi kama hicho mwaka 2015 na ikilinganishwa na uwiano wa chini
unaohitajika kisheria wa asilimia 20. Amana za wateja katika mabenki zilipungua kidogo kutoka
shilingi trilioni 20.73 mwezi Desemba 2015 kufikia shilingi trilioni
20.57 mwezi Septemba 2016. Miongoni mwa sababu zilizochangia kupungua
kwa amana kwenye mabenki ni pamoja na uamuzi wa Serikali kuhamisha
sehemu ya fedha za taasisi na mashirika ya umma kutoka mabenki ya
biashara kwenda Benki Kuu ya Tanzania. Hata hivyo, amana za serikali
kwenye mabenki ya biashara ni asilimia 3 tu ya amana zote za
mabenki. Aidha, jumla ya rasilimali za mabenki zimeendelea kuongezeka
kutoka shilingi bilioni 26,917.2 mwezi Desemba 2015 hadi kufikia
shilingi bilioni 27,978.2 mwezi Desemba 2016, sawa na ongezeko la
asilimia 2.6.
Mikopo kwa Sekta Binafsi
Mheshimiwa Spika,
mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka kwa asilimia 7.2 katika kipindi
cha mwaka ulioishia Desemba 2016 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia
24.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2015. Kupungua
kwa kiwango cha ukuaji kulitokana na tahadhari iliyochukuliwa na
mabenki kufuatia kuongezeka kwa mikopo chechefu kutoka asilimia 6.4
Desemba, 2015 hadi asilimia 9.5 Desemba, 2016.
Mheshimiwa Spika, ni vema pia ieleweke kuwa kupungua
kwa kasi ya kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi katika miezi ya
hivi karibuni siyo kwa Tanzania pekee. Kwa mfano, kiwango cha ukuaji wa
mikopo kwenda sekta binafsi katika nchi jirani ya Kenya kilipungua kutoka
asilimia 19.7 kati ya Julai na Oktoba 2015 hadi kufikia asilimia 4.1
katika kipindi kama hicho mwaka 2016. Aidha, Nchini Uganda mikopo kwa
sekta binafsi ilipungua kutoka asilimia 25.2 mwezi Septemba 2015 hadi
asilimia -1 mwezi Septemba 2016. Pia mwenendo usioridhisha ulijitokeza
katika mikopo chechefu katika nchi hizo jirani na kusababisha baadhi ya
mabenki hususan Crane Bank ya Uganda kuwekwa chini ya uangalizi. Hali ni
mbaya zaidi kwa nchi kama Nigeria na Ghana zinazouza mafuta.
Mheshimiwa Spika, upatikanaji
wa huduma za kifedha kwa wananchi wasiofikiwa na mabenki umeendelea
kuongezeka kutokana na ubunifu wa mipango ya utoaji wa huduma za malipo
ya rejareja kupitia simu za mikononi, pamoja na huduma za uwakala wa
mabenki (agent banking services).
Benki zilizopata msukosuko katika robo ya kwanza
Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha Julai – Desemba 2016, CRDB na TIB Development Bank zilipata
hasara. Hasara ilisababishwa na tengo kwa ajili ya mikopo chechefu
(provision for non performing loans). Aidha, Twiga Bancorp imewekwa
chini ya uangalizi wa BOT, jambo ambalo si geni. Crane Bank Ltd ya
Uganda iliwekwa chini ya usimamizi wa Benki Kuu ya nchi hiyo Oktoba 2016
kama ilivyokuwa Imperial Bank Kenya, Oktoba 2015. Licha ya hali hiyo,
benki nyingi zikiwamo CRDB na TIB Development Bank, zimebaki kuwa na
mitaji na ukwasi wa kutosha kwa mujibu wa Sheria. Aidha ni vema
kukumbuka kwamba jumla ya benki na taasisi za fedha nchini kote ni 66 na
zina matawi 783. Hivyo, kwa benki tatu (3) tu kupata msukosuko katika
robo moja ya mwaka si sababu ya kuzua taharuki. Ikumbukwe pia kuwa hiki
ni kipindi cha mpito na taasisi nyingi za Kibenki zilikuwa zinafanya
tathmini ya utekelezaji wa maamuzi ya Serikali ya kuyataka Mashirika na
Taasisi za umma kufungua akaunti za mapato BOT na kuhamishia amana za
taasisi hizo hususan akiba za muda maalum (fixed deposit) kutoka kwenye
mabenki ya biashara. Matarajio ya Serikali ni kuwa mara utaratibu mpya
utakapozoeleka shughuli za kiuchumi zitaendelea katika uhalisia wake na
Benki zitaendelea na huduma za mikopo na hivyo kuongeza ukwasi katika
Uchumi.
Uamuzi
wa Serikali Kuzitaka Taasisi za Umma Kufungua Akaunti za Mapato Benki
Kuu kama sababu ya Kupungua kwa Ukwasi katika uchumi.
Mheshimiwa Spika, ni
vyema Waheshimiwa Wabunge na jamii ya Watanzania ikafahamu kwamba
akaunti ambazo fedha za mashirika zimehamishiwa Benki Kuu ni akaunti za
kukusanya mapato tu na amana za muda maalum. Akaunti za matumizi bado
ziko katika benki za biashara ili kuyawezesha mashirika kufanya malipo
kupitia akaunti hizo. Hivyo, bado benki za biashara ni kiungo muhimu
kati ya mashirika ya umma na watoa huduma kwa mashirika hayo. Hatua
iliyochukuliwa na Serikali inalenga kuzisukuma benki za biashara
kuchukua hatua za ziada kupanua huduma za kifedha hadi vijijini badala
ya kujikita mijini zaidi kuhudumia makampuni makubwa (corporate sector)
na kufanya biashara katika soko la dhamana na hati fungani za Serikali.
Uamuzi huu umesaidia katika usimamizi wa mapato na matumizi ya
Mashirika hayo na pia kurahisisha upatikanaji wa taarifa za fedha
kupitia Benki Kuu. Aidha, Serikali imeacha kukopa fedha zake yenyewe na
kwa gharama kubwa. Kwa kuwa amana za Serikali kwenye mabenki ya biashara
ni sehemu ndogo tu (asilimia 3) ya amana zote za mabenki, madai kwamba
uamuzi wa Serikali kuondoa fedha za mashirika na taasisi kwenda kwenye
akaunti za mapato BOT umesababisha kupungua kwa ukwasi hayana uzito.
Mheshimiwa Spika,
naomba kusisistiza kuwa uamuzi wa Serikali kuzitaka taasisi za umma
kufungua akaunti ya mapato Benki Kuu utaendelea kubaki kama ulivyo. Kwa
kifupi, fedha hizi za umma zilikuwa zinatumika vibaya na mashirika
lakini pia zilitumika kuikopesha Serikali fedha zake yenyewe kwa riba
kubwa kupitia biashara ya dhamana na hati fungani za Serikali. Kasoro
hiyo iliondoa motisha kwa mabenki ya biashara kupeleka huduma za kifedha
vijijini na hata kukopesha sekta binafsi (crowding out credit to the
private sector).
Utoaji wa fedha kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2016
Mheshimiwa Spika, Serikali
inatambua umuhimu wa kupeleka fedha katika Halmashauri zetu kwa kuwa
ndiko utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma mbalimbali
kwa wananchi unapofanyika. Katika robo ya kwanza ya mwaka 2016/17,
Serikali ilipeleka jumla
ya shilingi bilioni 114.7 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya
maendeleo na matumizi mengineyo. Aidha, katika robo ya pili ya mwaka,
Serikali iliongeza mgao wa fedha zilizoenda kwenye Halmashauri ambapo
kiasi cha shilingi bilioni 203.4 zilipelekwa. Serikali itaendelea
kupeleka fedha katika halmashauri kwa kipindi kilichobaki kulingana na
bajeti iliyoidhinishwa na Bunge lako Tukufu ili kuhakikisha ufanisi
katika utekelezaji wa shughuli za halmashauri za kuwahudumia wananchi.
Ulipaji wa Madai Mbalimbali
Mheshimiwa Spika, hadi
kufikia Juni 30, 2016 kiasi cha shilingi bilioni 3, 113.7
ziliwasilishwa ikiwa ni madai ya wakandarasi, watumishi, wazabuni na
watoa huduma. Baada ya Serikali kufanya uhakiki kupitia kwa Mkaguzi wa
Ndani Mkuu wa Serikali ilibainika kuwa madai halali yalikuwa shilingi
bilioni 2,934.2 na madai yaliyokosa vielelezo na hivyo kukosa uhalali
yalikuwa shilingi bilioni 179.5.
Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha nusu mwaka wa 2016/17, Serikali imelipa jumla ya shilingi
bilioni 600.2. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 42.35 zilikuwa ni
kwa ajili ya madai ya watumishi, shilingi bilioni 49.46 kwa ajili ya
wazabuni, shilingi bilioni 11.2 kwa ajili ya watoa huduma, shilingi
bilioni 30.0 kwa ajili ya madai ya vyombo vya ulinzi na usalama, na
shilingi bilioni 467.2 kwa ajili ya wakandarasi mbalimbali ikijumuisha
shilingi shilingi bilioni 2.0 kwa ajili ya makandarasi wa maghala na
skimu za maji.
Mheshimiwa Spika, kuhusu
madeni ya pembejeo, Serikali bado inaendelea na uhakiki wa madeni hayo
ili kubaini madai halali na yasiyo halali. Hata hivyo, katika kipindi
cha Julai – Desemba, 2016 Serikali imetoa jumla ya shilingi bilioni 10.0
kwa ajili ya ruzuku ya pembejeo. Aidha, katika kuhakikisha madai ya
wakandarasi, wazabuni, watumishi na watoa huduma wa ndani wanapewa
kipaumbele, Serikali imeweka mkakati wa kutenga fedha kila mwezi ambapo
mwezi Januari 2017 Serikali imetenga jumla shilingi bilioni 70.0.
Jedwali Na. 2: Madeni yaliyolipwa kwa kipindi cha Julai - Desemba, 2016
Jedwali Na. 3: Deni lililobaki baada ya malipo ya hadi Desemba 2016
Mwenendo wa Deni la Taifa
Mheshimiwa Spika,
Deni la Taifa linajumuisha mikopo ambayo hukopwa na Serikali kutoka nje
na ndani ya nchi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo pamoja na
kujaza nakisi ya bajeti. Deni la nje hukopwa kutoka kwenye taasisi za
kifedha kama vile Benki ya Dunia, nchi Wahisani na pia kutoka kwenye
benki za biashara wakati deni la ndani linapatikana kwa kuuzwa kwa
dhamana za Serikali (treasury bills) na hatifungani (Treasury bonds),
mikopo kutoka Benki Kuu ya Tanzania na benki za biashara za ndani.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia Deni la Taifa kwa kuzingatia Sheria ya Mikopo, Dhamana, na Misaada
SURA 134. Aidha, katika kuhakikisha kuwa Deni la Taifa linasimamiwa
kikamilifu Serikali inakamilisha mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya
Mikopo, Dhamana na Misaada SURA 134 ili kuimarisha usimamizi wa Deni la
Taifa.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Desemba,
2016, Deni la Taifa likijumuisha deni la ndani na la nje lilifikia Dola
za Kimarekani milioni 19,021.9 (debt stock) ikilinganishwa na Dola za
Kimarekani milioni 18,459.3 Juni, 2016 ikiwa ni sawa na ongezeko la
asilimia 3.05. Kiasi hiki cha deni hakijumuishi deni la Mifuko ya
Hifadhi ya Jamii linalokadiriwa kufikia Dola za Kimarekani milioni
1,725.8 ingawaje deni hilo limezingatiwa katika tathmini ya uhimilivu wa
deni la Taifa.
Mheshimiwa Spika, ongezeko
la deni hilo limetokana na mikopo iliyopo na mipya iliyopokelewa na
Serikali na ambayo bado haijaiva kutoka mikopo ya ndani na nje ya nchi
kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile reli ya
Tazara, daraja la Kikwete mto - Malagarasi, barabara ya Morogoro –
Dodoma, barabara ya Dodoma – Singida – Arusha, barabara ya Mwanza –
Bukoba, mradi wa Maji ziwa Victoria, Bomba la Gesi Mtwara – Dar es
Salaam, barabara ya Dodoma - Singida – Mwanza, miradi ya umeme Kinyerezi
I & II, Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano n.k. Miradi ambayo
iligharamiwa na mikopo hiyo imeelezewa kwa kina katika kitabu cha
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2017/18 na katika
kitabu cha Uchambuzi wa Deni la Taifa pamoja na miradi inayofadhiliwa na
deni hilo. Pamoja na miradi iliyotajwa, naomba kuweka mezani taarifa ya
Agosti,2016 ya uchambuzi wa Deni la Taifa na miradi yote iliyofadhiliwa
na deni hilo tangu uhuru.
Ulipaji wa Deni la Taifa
Mheshimiwa Spika,
ulipaji wa Deni la Taifa hauangalii ukubwa wa deni lililopo (stock of
debt) bali kadri deni linavyoiva (debt maturity). Hali ilivyo sasa
sehemu kubwa ya Deni la Taifa linaiva kwa kipindi cha muda mrefu (long
term maturity). Kutokana na hali hiyo, kwa wastani (average time to
maturity) wa deni lililopo sasa litaiva katika kipindi cha miaka
isiyopungua 11.9. Hali hii inaashiria kwamba athari zake kwenye bajeti
ziko chini (low refinance risk).
Mheshimiwa Spika,
Serikali imekuwa ikilipa madeni ya nje na ndani kwa mujibu wa mikataba.
Katika kipindi cha kuanzia Julai, 2016 hadi kufikia Desemba, 2016
Serikali ilitumia jumla ya shilingi bilioni 2,570.1 kulipia madeni ya
ndani na nje yaliyoiva. Kati ya kiasi hicho, malipo ya deni la ndani ni
shilingi bilioni 1,822.3 na deni la nje ni shilingi bilioni 747.8.
Malipo ya deni la ndani yanajumuisha malipo ya mtaji (rollover) ya
shilingi bilioni 1,367.1 na malipo ya riba ya shilingi bilioni 455.2
Mheshimiwa Spika,
dhamira ya Serikali ni kuendelea kulipa kwa wakati mikopo yote ya nje
inayoiva kwa mujibu wa mikataba. Aidha, Serikali itaendelea na utaratibu
wa kukopa kwa ajili ya kulipa mtaji kwa amana zinazoiva (rollover of
principal maturities of T-bonds and T-bills). Lengo la kuendelea na
utaratibu huo (rollover) ni kutoa ahueni kwenye bajeti ya kila mwaka
husika na ni utaratibu wa kawaida unaotumika na nchi nyingi duniani.