Jacques Bihozagara alihudumu wakati mmoja kama balozi Ubelgiji
Serikali ya Rwanda
imeitaka Burundi kutoa ufafanuzi kuhusu kifo cha waziri wa zamani wa
Rwanda aliyefariki baada ya kuzuiliwa na Burundi kwa miezi minne
akituhumiwa kufanya ujasusi.
Jacques Bihozagara, aliyekuwa wakati mmoja waziri na balozi wa Rwanda,
alifariki tarehe 30 Machi, muda mfupi baada ya ufikishwa katika zahanati ya gereza la Mpimba.
Chanzo cha kifo chake hakijatangazwa rasmi.
Mkurugenzi
anayeangazia masuala ya Afrika katika wizara ya mambo ya nje ya Rwanda
Eugene Ngoga, amesema: “Jacques Bihozagara ni mmoja tu kati ya
Wanyarwanda wengi nchini Burundi ambao wamefariki katika hali
isiyoeleweka katika kipindi cha miezi saba iliyopita. Wizara ya Mambo ya
Nje ya Rwanda inataka maelezo ya ufasaha kutoka kwa watawala Burundi
kuhusu hali iliyopelekea kifo cha Bw Bihozagara na ufafanuzi kuhusu
sababu za kuzuiliwa kwake tangu Desemba mwaka jana”.
Rwanda pia imeitaka Burundi kusaidia familia ya marehemu kusafirishwa mwili wake hadi nyumbani kwake.
Balozi wa Rwanda nchini Ubelgiji alikuwa awali ameandika na kusema kifo cha Jacques kilikuwa ni "mauaji".
Umoja
wa Mataifa umekuwa ukiishutumu Rwanda kwa kujaribu kuipindua serikali
ya Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza, madai ambayo Rwanda imekuwa
ikiyakanusha.
Post a Comment