0

 
 
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, Betty Mkwassa.
 
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, Betty Mkwassa ametangaza operesheni ya kuwakamata wafugaji wavamizi katika wilaya hiyo na kuiweka alama mifugo ya wafugaji wa asili.
 
Lengo la kuendesha operesheni hiyo ni kubaini idadi ya ng’ombe waliopo ili kupanga matumizi bora ya ardhi kwa mfugaji kutoka kwenye ufungaji wa kuhama hama kwenda ufugaji kisasa.
 
Mkwasa alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kutoka Chama cha Waandishi wa Habari za Kilimo na Wafugaji (TAJF) waliotembelea wilayani ya Mvomero.
 
Alisema migogoro ya ardhi ilianza kuibuka katika Wilaya ya Mvomero mwaka 2004, lakini ameshangazwa  katika kipindi hicho imeshindwa kupatiwa ufumbuzi.
 
Alisema tagu kuhamishiwa katika wilaya hiyo,   kupitia wataalamu, walifanya utafiti na kubaini kuwa migogoro hiyo inasababishwa na mashamba pori na visasi baina ya wafugaji na wakulima.
 
“Halmashauri imeomba hati za mashamba 36 kufutwa lakini hadi sasa yamefutwa mashamba pori saba tu," alisema Mkwasa. "Mashamba makubwa yamekuwa kitendawili kufutwa.”
 
Alisema wanajipanga kuendesha operesheni hiyo ili baadaye wilaya itoe mikataba kwa watendaji wa vijiji na kata kutoruhusu mifugo mipya kuingia katika vijiji vyao.
 
“Nafahamu mbinu hii itatusaidia kudhibiti ongezeko la mifungo, hivyo kiongozi atakayeshindwa kutekeleza  wajibu huo atachukuliwa hatua za kinidhamu kwa kukiuka makubaliano,” alisema.
 
Mmoja wa wafugaji wa kijiji cha Kambala, George Payana alisema serikali inapaswa kufanya maadilizi  kabla ya kuendesha operesheni ya kupunguza idadi ya mifugo.
 
Alisema suala hilo linaweza kuwa rahisi ikiwa serikali itajenga malambo na majosho na kutoa elimu kwa wafugaji kwa hiari yao wapunguze mifugo wenyewe.
 
“Unajua serikali hutumia ubabe kupunguza mifugo bila  ya kumshirikisha mfugaji," alisema Payana na kuomba "utaratibu huo usitumike kwenye operesheni hiyo ili kudumisha amani na upendo.”
 
Alisema lazima ifahamike kuwa hakuna mgogoro kati ya wafugaji na wakulima kwa sababu wote wanategemeana kiuchumi na kijamii.
Migogoro hiyo, alisema Payana, hutengenezwa kwa maslahi ya wenye mashamba makubwa walioshindwa kuyaendeleza, wakiwamo wanasiasa.
 

Post a Comment

 
Top