0

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)
 
Yanga imelipiga bao Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), baada ya shirikisho hilo kukubali kimya kimya kupangua ratiba ya mechi ya kiporo iliyopangwa kufanyika katikati ya wiki hii.
Yanga ilikuwa ipambane na Mtibwa Jumatano wiki hii, lakini mechi hiyo haitakuwapo na TFF itapanga tarehe nyingine ya kuchezwa.
 
Hata hivyo, habari kutoka TFF zilidai kuwa mchezo huo utachezwa baada ya Yanga kucheza mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly wikiendi ijayo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
 
Kabla ya kusogezwa mbele mchezo huo, Yanga na Azam FC zinazoshiriki michuano ya klabu Afrika ziliomba kufanywa kwa marekebisho ya ratiba ya mechi za viporo, wakidai kuwa watalazimika kucheza mechi mfululizo hivyo kukosa nafasi ya kujiandaa na mechi za kimataifa.
 
Hata hivyo, TFF kupitia Bodi ya Ligi ilikataa kupangua ratiba hiyo na kuzitaka timu hizo kujipanga kwa ratiba hiyo iliyozibana na kuzitaka kucheza mechi nne ndani ya siku 10.
 
Hata hivyo, taarifa za jana zilithibitisha TFF kupangua ratiba ya mechi za kiporo kwa mchezo mmoja tu wa Yanga dhidi ya Mtibwa, huku mechi za Azam FC zikibaki kama zilivyopangwa.
 
Msemaji wa Azam FC, Jaffer Idd alisema jana kuwa wamejipanga kucheza mechi za viporo kama ratiba inavyoonyesha.
 
"Tangu bodi ya Ligi ilipokataa kukaa mezani na sisi kuzungumzia malalamiko yetu kuhusu ratiba ngumu ya mechi za viporo, tuliamua kujipanga na tunaendelea na ratiba kama kawaida. Hakuna mechi yetu iliyosogezwa mbele," alisema Idd.

Post a Comment

 
Top