0

Kocha Boniface Mkwasa.
 
Kocha Boniface Mkwasa, amesema yuko tayari kufundisha timu yoyote, lakini tu kama waajiri wake wa sasa - Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) watapewa taarifa.
 
Mkwasa kwa sasa anafundisha timu ya Taifa (Taifa Stars) na kauli yake imekuja siku chache tangu kuwalalamikia waajiri wake (TFF) kushindwa kumlipa misharaha kwa miezi nane.
 
Kocha huyo mzawa, anaidai TFF Sh. milioni 200 ambazo ni malimbikizo ya mishahara tangu Julai mwaka jana.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkwasa aliyetua Stars akitoka Yanga, alisema yuko tayari kwenda kufundisha timu yoyote itakayomuhitaji.
 
Alisema pamoja na kwamba aliachana na ajira yake Yanga, lakini haina maana kwamba lazima arudi alikotoka.
 
"Niko tayari kufanya kazi na timu yoyote itakayonihitaji, siyo lazima nirudi Yanga. Naweza kwenda popote," alisema Mkasa.
Kauli ya Mkwasa ilikuja baada ya kuwapo na taarifa kuwa ameamua kurudi Yanga.
 
"Siyo kwenda, siwezi kwenda Yanga kwa sababu nina mkataba na TFF. Kama kuna klabu inanihitaji, basi wawasiliane na mwajiri wangu wa sasa (TFF)," alisema.
 
Alisema hana taarifa za kuitwa Yanga na kama hilo lipo, basi atajulishwa na kusisitiza kuwa, siyo lazima kurudi Yanga.
 
Msemaji wa Yanga, Jerry Muro alisema jana kwa sasa hawana mpango kuongeza kocha kwenye kikosi chao zaidi ya kuelekeza nguvu kwenye michuano ya ligi kuu na kimataifa.

Post a Comment

 
Top