Kocha Mkuu wa Yanga Hans van der Pluijm
TFF ilitoa ratiba ya mechi za viporo kwa timu za Yanga na Azam, ambazo pia zinaiwakilisha nchi kwenye michuano ya Klabu Afrika.
Marekebisho hayo ya ratiba yamelalamikiwa na timu zote na TFF imeshikilia msimamo wake wa kutopangua tena ratiba.
Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm alisema jana kuwa marekebisho hayo yaliyofanywa na TFF ni sawa na hujuma kwao.
Alisema ratiba hiyo ni ngumu kwao na inalenga kuwapoteza kwenye mbio za kutetea ubingwa wao.
"Ratiba hii haitupi nafasi ya kutetea ubingwa wetu wa Bara wala
kwenda hatua ya makundi Ligi ya Klabu Bingwa Afrika," alisema Pluijm.
Juzi Machi 31, Yanga ilicheza mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya
Ndanda FC, kesho itaikaribisha Kagera Sugar na Jumatano itawakabili
Mtibwa Sugar kwenye mechi za Ligi Kuu, huku ikishuka uwanjani Jumamosi
ijayo kupambana na Al Ahly ya Misri.
Akizungumza na Nipashe jana, Pluijm alisema hata kama mechi zote
nne zinafanyika kwenye uwanja wa nyumbani, bado ratiba ni ngumu kwetu.
Pluijm alisema wachezaji wa Afrika hawakuandaliwa kucheza mechi
nyingi kwa muda mfupi na hiyo ilitokana na uwezo wao wa kuhimili
ushindani unaosababishwa na mazingira waliyokulia kwenye mchezo huo.
"Hali hii si nzuri kwa upande wetu, hata kama ukicheza mechi nyingi
timu inakuwa imara, wakati huohuo wachezaji wanachoka, inawafanya
wachezaji watumie zaidi uzoefu na si kuonyesha viwango vizuri kama
wangepata muda wa kupumzika, namna hii ni hatari, ukipoteza umakini
kidogo unampa nafasi mpinzani kutumia makosa yako," alisema kocha huyo.
Aliongeza kama ligi ilisimama kupisha maandalizi ya timu ya taifa
ilipokuwa inajiandaa kuikabili Algeria, pia kwa uzito uleule ilipaswa
Yanga na Azam FC zinazoshiriki ya kimataifa kupewa muda wa kujinoa.
"Ni hatari kucheza mechi nyingi za mashindano tofauti kwa wakati mmoja," Pluijm aliongeza.
Aliongeza kuwa uzoefu ndiyo uliwasaidia wachezaji wake kupata
ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ndanda FC katika mechi ya hatua ya robo
fainali iliyofanyika juzi.
Kocha huyo pia aliwataja wachezaji wake wawili wa kimataifa, Amissi
Tambwe na Haruna Niyonzima tayari wamewasili nchini na kujiunga na
kikosi cha timu hiyo.
Tambwe alikuwa Namibia na timu yake ya taifa ya Burundi, wakati Niyonzima ametokea Rwanda iliyocheza dhidi ya Mauritius.
Post a Comment