Maombi na furaha ya watanzania wote wazalendo ni kuona Yanga ikifanikiwa kuingia katika hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la shirikisho barani Afrika CAF, licha ya kuwa nafasi yao kwa sasa inatajwa kuwa ndogo, lakini Yanga wanayo nafasi ya kusonga mbele licha ya kuwa na point moja na wapo mkiani.
Safari ya Yanga kutinga hatua ya nusu fainali ya CAF inamlazimu ashinde mechi zake zote mbili zilizosalia za MO Bejaia atakayocheza nyumbani na mechi dhidi ya TP Mazembe atakayocheza ugenini, huku akiombea mechi ya mwisho kati ya MO Bejaia ya Algeria dhidi ya Medeama imalizike kwa sare ya aina yoyote ile.
TP Mazembe bado imeendelea kuipa matumaini Yanga baada ya mchezo wa leo kufanikiwa kuifunga MO Bejaia kwa goli 1-0, goli ambalo lilifungwa na Rainford Kalaba dakika ya 62, kwani kama TP Mazembe angefungwa leo Yanga wangekuwa rasmi wameaga michuano hiyo wakiwa wamesalia na michezo yao miwili mkononi.