Mkurugenzi
wa Usimamizi wa Uchumi wa amlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji
(Ewura), Felix Ngamlagosi akitangaza bei mpya ya umeme jana katika
mkutano na waandishi wa Habari Dar es Salaam. Kulia kwake ni Mkurugenzi
wa Umeme wa mamlaka hiyo, Anastas Mbawala. (PICHA NA RICHARD MWAIKENDA
TAARIFA KAMILI
Tarehe
11 Oktoba 2013, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) liliwasilisha
maombi ya kurekebisha bei ya umeme kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za
Nishati na Maji (EWURA). TANESCO ilipendekeza kuongeza bei kwa asilimia
67.87 kuanzia tarehe 1 Oktoba 2013, asilimia 12.74 kuanzia tarehe 1
Januari 2014 na asilimia 9.17 kuanzia tarehe 1 Januari 2015. Vilevile
TANESCO waliomba kuidhinishwa kwa kanuni ya kurekebisha bei ya umeme
kulingana na mabadiliko ya bei za mafuta, mfumuko wa bei na mabadiliko
ya thamani ya shilingi ya kitanzania. Aidha, TANESCO iliomba
kuidhinishwa viwango vya gharama za kuunganisha umeme vinavyozingatia
ruzuku inaliyotolewa na Serikali, na kuidhinishwa tozo mbalimbali kwa
huduma zitolewazo na TANESCO.
Kwa
mujibu wa TANESCO, kupitishwa kwa maombi haya kutaliwezesha Shirika (a)
kupata fedha za uendeshaji na uwekezaji wa miundombinu, (b) kulifanya
Shirika liweze kukopesheka na hivyo kuwezesha kupata mikopo yenye
masharti nafuu, (c) kuliwezesha Shirika kukabiliana na ongezeko la
mahitaji ya umeme kwenye Gridi ya Taifa, na (d) kuongeza uwezo wa
kufanya matengenezo ya mara kwa mara ya miundombinu iliyopo ili
kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa huduma za umeme wa uhakika kwa
wateja.
Itakumbukwa
kwamba bei za umeme zinazotumika hivi sasa ziliidhinishwa mwezi Januari
2012. Bei hizo zilipanda kwa asilimia 40.29 ikilinganishwa na maombi ya
TANESCO ambapo ilipendekeza bei zipande kwa wastani wa asilimia 155.
Sababu ilikuwa ni kuongezeka kwa gharama za uendeshaji kulikosababishwa
na hali ya ukame katika maeneo yanayotiririsha maji katika mabwawa ya
kuzalishia umeme, toka mwaka 2011. Hali hiyo ilipelekea TANESCO
kulazimika kununua umeme kwa gharama kutoka kwa wazalishaji wa dharura
(Emergency Power Producers). Hali ya maji katika mabwawa ya kuzalishia
umeme bado sio nzuri na hivyo TANESCO itaendelea kununua umeme kutoka
kwa wazalishaji wa dharura (Emergency Power Producers).
USHIRIKISHWAJI WA WADAU
Kulingana
na Kifungu Na. 19(2) (h) cha Sheria ya EWURA, Mamlaka ilifanya Taftishi
ili kupata maoni juu ya ombi la kurekebisha bei za umeme. Ukusanyaji wa
maoni ulihusisha pia mikutano minne (4) iliyofanyika Iringa na
Shinyanga tarehe 15 Novemba 2013, Bagamoyo tarehe 20 Novemba na
kuhitimishwa Dar es Salaam tarehe 22 Novemba 2013. Aidha, tarehe 6
Desemba 2013, EWURA iliitisha mkutano wa mwisho wa wadau wakiwemo
wawakilishi kutoka Wizara ya Nishati na Madini(MEM), TANESCO, Shirika la
Umeme la Zanzibar (ZECO), Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania, Baraza
la Watumiaji na Baraza la Ushauri la Serikali, Umoja wa Wazalishaji wa
Saruji wa Afrika Mashariki, na kiwanda cha ALAF. Katika mkutano huo
EWURA iliwasilisha mwelekeo wa maamuzi kuhusu maombi ya TANESCO na namna
zilivyokokotolewa. Wadau walipewa fursa ya kutoa maoni yao kuhusu
mwelekeo wa bei na maoni yao yamezingatiwa katika kufikia maamuzi ya
mwisho.
UCHAMBUZI NA UAMUZI
Kwa kufuata sheria na kanuni zinazoelekeza kuhusu uchambuzi wa bei ya
umeme, EWURA ilifanya uchambuzi wa kifedha na kiufundi ili kubaini uwezo
wa TANESCO katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku. Uchambuzi
uliangalia utendaji wa Shirika la TANESCO katika miaka iliyopita na pia
iliangalia majukumu yanayoikabili TANESCO katika miaka mitatu ijayo.
EWURA imebaini kwamba hali ya kifedha ya Shirika la Umeme sio nzuri.
Shirika limeendelea kupata hasara, ambayo iliongezeka kutoka shilingi
bilioni 47.3 katika mwaka 2010 na kufikia shilingi bilioni 223.4
mwishoni mwa mwaka 2012. Pamoja na mapungufu ya kiufanisi, sababu kubwa
ya ongezeko la hasara ni kuongezeka kwa gharama za uzalishaji wa umeme
ambao TANESCO inanunua kutoka kwa wazalishaji binafsi. Hali hii
imelifanya shirika kushindwa kulipa madeni yake ya muda mfupi na ya muda
mrefu, ambayo yamelibikizwa na kufikia TZS 456.8 bilioni tarehe 22
Novemba 2013, hali ambayo inatishia uendelevu wa huduma ya umeme hapa
nchini.
Mamlaka imetumia Kanuni ya Ukokotoaji wa Bei kama ilivyopendekezwa na
AF-MERCADOS wakati wa kukokotoa mahitaji ya mapato ya TANESCO. Kanuni
hiyo inawezesha kukokotoa bei zinazolandana na gharama halisi kwenye
mfumo wa umeme na kuzigawa kwenye makundi ya watumiaji umeme, kadiri
kila kundi linavyosababisha gharama kwenye mfumo wa umeme kwa mujibu wa
mahitaji ya Sheria ya Umeme ya 2008 Kifungu cha 23(2)(f).
EWURA imejiridhisha kwamba, ufumbuzi wa matatizo ya kifedha ya TANESCO, unahitaji njia/mikakati miwili itekelezwe kwa pamoja:
kuongeza bei ya umeme ili kufikia bei inayokidhi gharama halisi (Cost Reflective Tariff); na
TANESCO kupata mkopo wa gharama nafuu ama ruzuku kutoka Serikalini ili kulipa limbikizo la madeni ya Shirika.
Bodi ya Wakurugenzi wa EWURA, katika kikao chake cha tarehe 10 Desemba
2013 pamoja na mambo mengine, ilitoa maamuzi ya ongezeko la bei za umeme
kwa viwango mbalimbali kwa makundi mbalimbali ya wateja, kama
ifuatavyo:
Kundi D1: Hili ni kundi la wateja wadogo wa majumbani, hasa
vijijini, ambao hutumia wastani usiozidi wa Uniti 75 kwa mwezi. EWURA
imeongeza wigo wa mahitaji ya umeme na kufikia uniti 75 kwa mwezi, lengo
likiwa ni kuongeza idadi ya wateja wa TANESCO wanaoweza kulipa kidogo
kwa matumizi ya umeme kwa kiwango hicho, na pia kuwahamasisha kutumie
zaidi umeme. Awali kundi hili lilikuwa linatunia wastani wa matumizi ya
uniti 50 kwa mwezi. Bei mpya ni shilingi 100 kwa uniti moja, kutoka
shilingi 60 za sasa, sawa na ongezeko la shilingi 40.
Kundi T1: Hili ni kundi la watumiaji wakubwa wa umeme majumbani,
biashara ndogondogo, mashine za kukoboa na kusaga nafaka, taa za
barabarani, mabango n.k. Bei iliyoidhinishwa ni shilingi 306 kwa uniti
moja, ikiwa ni ongezeko la Shilingi 85 ya bei ya sasa. TANESCO
ilipendekeza ongezeko la shilingi 131.
Kundi T2: Hili ni kundi la watumiaji umeme wa kawaida ambao
hupimwa katika msongo wa volti 400, na ambao matumizi yao ya wastani kwa
mwezi ni zaidi ya uniti 7,500 wateja wafanyabiashara kubwa, viwanda vya
kati. Bei ya nishati iliyoridhiwa ni shilingi 205 kwa uniti moja, sawa
na ongezeko la shilingi 73 ya bei ya sasa. TANESCO walipendekeza
ongezeko la shilingi 145 ya bei ya sasa.
Kundi T3-MV: Hili ni kundi la wateja wakubwa kama viwanda vikubwa
waliounganishwa katika msongo wa kati (Medium Voltage). EWURA
imeidhinisha bei ya nishati kwa kiwango cha shilingi 166 kwa uniti moja,
sawa na ongezeko la shilingi 45 ya bei ya sasa. TANESCO walipendekeza
ongezeko la shilingi 148 kwa uniti moja.
Kundi T3-HV: Hili ni kundi la wateja wakubwa waliounganishwa
katika msongo wa juu (High Voltage – Voti 66,000 na zaidi) ikiwa ni
pamoja na ZECO, Bulyanhulu, na Twiga Cement. Bei iliyoidhinishwa ni
shilingi 159 kwa uniti moja, sawa na ongezeko la shilingi 53 la bei ya
sasa. TANESCO waliomba ongezeko la shilingi 80 kwa uniti moja.
Bei ya umeme itakuwa inarekebishwa kila baada ya miezi mitatu kulingana
na mabadiliko ya kiwango na bei za mafuta; mfumuko wa bei, mabadiliko ya
thamani ya fedha, na upatikanaji wa ruzuku toka Serikalini.
Vilevile, TANESCO inatakiwa kutekeleza miradi ya uwekezaji iliyoainishwa
kwa kutumia fedha zitakazokusanywa kutokana na bei zilizoidhinishwa.
EWURA inaweza kurekebisha bei ya umeme ya TANESCO kila mwisho wa mwaka
2014 na/au mwaka 2015 endapo TANESCO itashindwa kutekeleza miradi
iliyotajwa katika Jedwali husika. Marekebisho hayo yatatokana na
makadirio ya gharama za miradi ambayo haikutekelezwa.
Kutokana na matazamio ya kuwa na mabadiliko makubwa katika uzalishaji wa
umeme (generation mix) katika mwaka 2015 na kuendelea, kutokana na
matarajio ya kuongezeka kwa kwa upatikanaji wa gesi asilia, EWURA
itafanya utafiti kubaini gharama halisi (Cost of Service Study) ya
huduma ya umeme kwa wakati huo. Hivyo, bei zilizoidhinishwa zitatumika
mpaka mwaka 2016, kama utafiti unaotazamiwa kufanywa hautakamilika kabla
ya mwisho wa mwaka 2015.
EWURA ililinganisha bei za umeme kwa kila Uniti, katika nchi za Afrika
ya Mashariki, na kuona kuwa bado bei za umeme za Tanzania zipo chini
ukilinganisha na bei za katika nchi jirani kama inavyoonyeshwa hapa
chini, kwa makundi mbalimbali ya watumiaji umeme.
Post a Comment