Mwenyekiti
wa kikao cha jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa, kinachoendelea
Arusha, Bernard Luanda, leo amegeuka mbogo kwa wanasheria wa serikali
kwa kitendo cha kumnyima Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema dhamana
kwa lengo la kumnyima haki.
Akizungumza
Mahakamani hapo leo mbele ya majaji wenzake Stella Mugasha na Jaji
Kipenka Mussa, Luanda amesema haipendezi na haingii akilini mtu (Lema)
kushikiliwa kwa miezi minne bila sababu kwa misingi ya kumnyima haki.
“Tunaomba
ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikai (DPP) muwe makini sana maana
mnatufanya wanasheria wote hatuna akili na mnachafua Mahakama, kwa hali
ya kawaida mtu mumshikilie kwa misingi ya kisheria, lakini katika kesi
hii tumepitia jalada hatujaona kitu chochote cha kumshikilia Lema hadi
leo na imetushitua sana,” alisema huku akishauriana na wenzake mara kwa mara kwa masikitiko.
Aliendelea kusema kuwa ofisi ya DPP inaitia najisi taaluma hiyo, kitu kipo wazi ila wanafanya vitu vya ajabu na havipendezi.
Alihoji jaji Luanda kuwa
“Tumesoma faili lote tunashangaa hivi kweli ofisi ya mwanasheria mkuu
ina wanasheria kweli na kama wapo kwa nini huyu mtu (Lema) awe ndani
mpaka leo?”.
Alisema
kwa kuwa mikono yao kisheria imefungwa hawawezi kufanya chochote kwa
leo na kuwataka Mawakili upande wa Lema kurudi Mahakama Kuu, kuendelea
na maamuzi ya dhamana.
Hali
hiyo ilitokana na Wakili wa serikali Faraja Nchimbi kusimama mahakamani
hapo na kuomba kuiondoa rufaa hiyo kwa madai kuwa ipo nje ya uwezo
wake.
“Waheshimiwa
Majaji baada ya timu yetu ya wanasheria kupitia kwa kina rufaa hii kwa
sababu zisizozuilika tumeona hatupo tayari kuendelea na rufaa hii, maana
hatukupeleka kusudio (Notisi) kwa msajili muda ulipita, hivyo tunaomba
kuiondoa na uamuzi wa kuiondoa rufaa hii tumeufikia Ijumaa muda uliisha
kuja mahakamani,”. Alisema Nchimbi.
Baada
ya kuwasilisha ombi hilo, Wakili wa Lema Peter Kibatala, alisimama na
kusema upande wao hawana pingamizi ila waliomba hoja za awali za rufaa
hiyo ziondolewe Mahakamani hapo bila kunakiliwa.
Baada ya ombi hilo Jaji Kipenka Mussa alipokea kwa niaba ya Majaji wenzake na kukubali ombi la kuiondoa rufaa hiyo namba 9/2017.
Aidha
Jaji Luanda alimkaribisha jaji Stella Mugasha pia kuongea kwa niaba yao
ambapo alisema mahakama imekubali ombi la pili la kuiondoa rufaa namba
10/2017, baada ya Wakili Paul Kadushi kuomba kuiondoa pia.
Wakili
wa Lema Peter Kibatala, alilazimika kusimama tena Mahakamani hapo
kusema kuwa upande wao unasikitika kuona ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali na DPP wanatumia Mahakama kwa njia ya kumnyima haki mteja wao,
hivyo aliomba mahakama hiyo iwatatulie tatizo la kisheria lililojitokeza
hadi mteja wao awe ndani hadi sasa.
Kibatala aliongea hayo huku akishindwa kujizuia na kumwaga chozi la huzuni mahakamani hapo mbele ya Majaji hao.
Post a Comment