HEDHI ni mzunguko wa kila mwezi ambao huleta kutokwa na damu ukeni kutokana na mimba kutotungwa. Kwa kawaida hedhi ya kwanza hutokea katika umri wa miaka 12 -13. Mzunguko huu wa hedhi huwa unadhibitiwa na homoni zinazozalishwa na mwili.
Hedhi hutokea pale ambapo tishu za ukuta wa mji wa mimba unabomoka na kutoka kama damu ukeni.
Kila mwezi ovari za mwanamke huzalisha yai moja la uzazi. Yai hili huweza kukaa kwa muda mpaka wa saa 36 ndani ya mirija na tumbo la uzazi. Inapotokea yai hili halijarutubiwa, ukuta wa mji wa uzazi hubomoka na kutoka kwa njia ya uke pamoja na damu. Hali hii huitwa hedhi.
Mzunguko wa hedhi huanza kuhesabiwa siku ya kwanza mwanamke anapoanza kupata siku zake.
Sasa basi, mwanamke anapoingia katika mzunguko huo anapaswa kuwa makini ili kuboresha afya yake.
Kwa sababu hiyo, mtandao wa asasi za kiraia wa Tanzania Water and Sanitation Network (TAWASANET) umeamua kutoa elimu shuleni kwa walimu na wanafunzi wa kike juu ya namna ya kujisitiri wakati wa hedhi.
Lengo ni kuhakikisha kwamba kadiri muda unavyosonga mbele huduma ya kujisitiri katika kipindi cha hedhi hasa kwa wasichana walioko shuleni inaangaliwa kwa ukaribu zaidi.
Mratibu wa TAWASANET, Emmanuel Jackson, anasema hedhi katika Bara la Afrika inachukuliwa kama jambo la siri na la aibu kabisa ambalo haliwezi kuzungumzwa na watu wala kulisema hadharani, katika mfumo huu jamii imekuzwa kiasi kwamba haiwezi tena kushughulikia changamoto zinazohusiana na hethi.
Jackson anasema ugumu wa kushindwa kushughulikia changamoto za hedhi kunawaathiri zaidi wasichana walioko shuleni, hii ni kwa sababu changamoto hizo zinagusa kwa namna moja ama nyingine mfumo wa kujifunza unaochangiwa na mazingira pamoja na miundombinu ya shuleni na mifumo iliyopo majumbani.
“Ili wanafunzi wa kike wawe na afya bora, shule zinapaswa kuwa na vyoo rafiki kwa wasichana, sehemu ya kubadilishia na kutunzia vihifadhio, (mfano pedi) maji safi, utaratibu mzuri wa usafi ikujumuisha unawaji mikono kwa sabuni, pamoja na ukaribu na walimu.
“Pasipo upatikanaji wa vifaa hivi ikijumuisha na mazingira rafiki kwa wasichana, ufaulu wa wasichana unabaki kuwa shakani,” anasema Jackson.
Huduma ya kujisitiri na ufaulu
Dk. Hamis Malebo, kutoka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), anasema mfumo mzuri wa kiafya shuleni ni ule ambao desturi na taratibu zinaandaliwa na kusimamiwa kwa kuliona suala la hedhi kuwa ni la aibu, matokeo yake msichana hapati ushirikiano wa kutosha katika mazingira ya nyumbani, shuleni na kwa jamii inayozunguka.
Anasema hii inamaanisha kwamba msichana anaachwa apambane na changamoto hizo peke yake hata kama hana uwezo kwa wakati huo kimwili, kiakili, kisaikolojia au hata kifedha.
Dk. Malebo anasema katika mfumo wa elimu wa sasa kwa maeneo mengi nchini, wasichana wanakabiliwa na gharama kubwa za kununua vihifadhio mfano pedi.
“Hii inasababisha wasichana kuchagua njia rahisi ambazo haziwahifadhi kwa ufanisi ama kutafuta njia mbadala (mfano kuwa na uhusiano na wanaume) ili wapate fedha za kutimiza mahitaji ikiwemo vihifadhio.
“Upungufu wa maji kwa ajili ya kuoga ama kujisafisha wakati wa kipindi cha hedhi, au kusafisha vihifadhio(kwa wanaotumia njia ya asili) hali hii inaongeza hofu kwa wasichana kuhisi kuwa watatoa harufu mbaya, ama kuwa na hisia kuwa hawako safi wanapokuwa kati ya wanafunzi wengine,” anasema Dk. Malebo.
Anasema uchafu wa vyoo ama visivyofaa kwa matumizi hasa kwa wasichana wanaoingia katika hedhi, huleta changamoto kubwa kwao.
Anasema kuvuja kwa hedhi kutokana na kutumia vihifadhio vilivyo katika viwango vya chini ni kitendo ambacho huwadhalilisha wasichana.
Dk. Malebo anasema kutokuwa na walimu wanaotoa msaada stahiki kwa wasichana walio katika hedhi mfano kuwapa ruhusa kwenda chooni au chumba cha kubadilishia wakati vipindi vya darasa vikiendelea ama kutokuwa na adhabu kali zinazoweza kuongeza uwezekano wa kudhalilika.
Anasema kutokana na msongo wa kuhisi aibu changamoto hizi husababisha wasichana shuleni kuchagua kubaki nyumbani na kutohudhuria masomo katika kipindi cha hedhi na wengine wameripotiwa kuacha kabisa masomo.
Inasemekana kuwa baadhi ya wasichana hukosa masomo kati ya siku moja hadi saba ama zaidi katika kipindi cha kila mwezi ambapo sababu kubwa zinazochangia ni pamoja na hofu ya kushindwa kudhibiti hedhi (kuvuja) hatimaye kudhalilika akiwa shuleni hasa anapotakiwa na mwalimu kuandika ubaoni akiwa na wenzake darasani.
“Wapo wengine ambao hukabiliwa na maumivu makali hasa katika siku mbili za awali hivyo hupungukiwa na uwezo wa kufuatilia masomo na wengine huwa na hali ya kutojisikia vizuri hatimaye kushindwa kuhudhuria masomo.
“Wengine hufanya siri hivyo njia rahisi inayochaguliwa ni kutofika shuleni ili wawe salama,” anasema Dk. Malebo.
Hali halisi ya mazingira ya shule
Mhandisi kutoka taasisi ya Water Supply and Sanitation Collaboretive Council (WSSCC) Wilhemina Malima anasema programu za elimu, ikijumuisha kwa shule za msingi na sekondari, zimeboresha kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi shuleni.
Anasema hata hivyo, uwiano hauko sawa baina ya udahili na uboreshaji wa miundombinu itakayokuwa rafiki hasa kwa wasichana wanapokuwa katika kipindi cha hedhi.
Nini kifanyike?
Ili kuweka mazingira mazuri zaidi ya ufaulu kwa wasichana walio shuleni, ni muhimu wanafunzi wawe na uhakika wa kupata pedi.
Hii inatokana na uhalisia wa hali duni ya kiuchumi wanayokabiliana nayo baadhi yao ambapo hushindwa kununua vihifadhio hatimaye kutafuta njia mbadala, endapo kama kutahitajika kuchangia uandaliwe utaratibu mzuri, mfano kwa wazazi au kwa wanajamii badala ya kuchangisha wasichana ambao hawana vyanzo vya mapato.
Pia Serikali inashauriwa kuidhimisha sehemu ya fedha ya ruzuku(Capitation Grant) kuchangia upatikanaji wa pedi, pia shule ziweke mipango ya upatikanaji wa fedha kwa ajili hiyo.
Pia elimu ya afya ya uzazi itolewe kwa wasichana ili waweze kujitambua na kujihifadhi vizuri hasa wanapokuwa katika kipindi cha hedhi, kwa waalimu ili kuongeza ujuzi namna ya kuwasaidia wasichana, kwa jamii ili waondokane na mila na desturi zinazowaathiri watoto.
Post a Comment