Kutengeneza kucha: Ajira inayowaweka majaribuni vijana
ENEO la Nyerere Square lililopo mkoani Dodoma ni maarufu mno kwa sababu ya kuwapo kwa sanamu ya Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere.
Mbali ya kuwa na sanamu hiyo, pia ni eneo la kibiashara ambapo kuna biashara za kila aina, kama za kuuza vocha na upigaji picha.
Pia kuna soko ambalo hufunguliwa nyakati za jioni tu ambapo hupatikana nguo, vito na viatu huku wauzaji wengi wakiwa ni vijana kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dodoma.
Biashara nyingine kubwa inayofanyika katika eneo hilo ni ile ya kupaka rangi, kubandika kucha pamoja kuosha miguu huku wateja wakiwa ni kina dada na akina mama kutoka maeneo mbalimbali.
Mwandishi wa makala haya anaamua kufunga safari mpaka katika eneo hilo na kufanya mahojiano na wafanyabiashara.
Dennis Batholomeo, anasema ameamua kujiajiri katika biashara ya kubandika kucha na kupaka rangi kutokana na ugumu wa maisha uliokuwa nyumbani kwao na kwamba kwa siku huwahudumia watu 20 mpaka 25.
“Mimi nimetoka Babati mkoani Manyara, hii biashara niliianzia Babati baadae ndio nikaja hapa Dodoma. Kwa siku huwa natengeneza watu zaidi ya 20,” anasema Batholomeo.
Anasema katika maeneo hayo biashara kubwa inayofanyika ni ya kubandika kucha, kuchora kucha pamoja na kuosha miguu kwa kina dada na kaka.
Anasema bei za kubandika kucha ni kati ya Sh 10,000 hadi 15,000 wakati kupaka rangi ni kati ya Sh 3,000 hadi 5,000 na kuosha miguu na mikono ni kati ya Sh 5,000 hadi 10,000.
“Kwa siku kipato chetu ni kuanzia Sh 80,000 na kuendelea, ila kipato huwa kinakuwa kikubwa siku za mwisho wa wiki kutokana na watu kuwa wengi,” anasema.
Naye Musa Kitoti anasema biashara ya kuchora kucha imemsaidia kujikwamua kimaisha kwa kuwa sasa anaweza kumsomesha mdogo wake aliyeko Kigoma.
“Nimetokea Kigoma, nilipokuwa shule nilikuwa na kipaji cha kuchora na leo kipaji hiki kimenisaidia naweza kubandika kucha vizuri pamoja na kupaka rangi.
“Nilikuwa na maisha magumu lakini sasa hivi nashukuru fedha ya kula haisumbui na mdogo wangu anaenda shule kutokana na kazi hii,” anasema Kitoti.
Naye Yohana Jackson, anasema ametoka mkoani Ruvuma kwa ajili ya biashara hiyo baada ya kushawishiwa na rafiki yake kuwa biashara hiyo inalipa mkoani Dodoma.
“Kuna rafiki yangu alikuja likizo mwisho wa mwaka akaniambia twende Dodoma biashara ya kubandika kucha na kupaka rangi inalipa, mimi sikujivunga niliamua kuja.
“Mwanzo nilikutana na changamoto nyingi lakini sasa hivi nimezoea, nimeoa na nina mke na watoto wawili ambao wana uhakika wa kusoma pamoja na kula kila siku kutokana na biashara hii,” anasema.
Anasema kwa siku huhudumia wateja kati ya 20 mpaka 30 kwa kupaka kucha, kuosha miguu pamoja na kubandika kucha katika mikono na miguu.
Kwa upande wake Lazaro Ikoa anasema biashara yao imekuwa kubwa kutokana na kuwapo kwa wanafunzi wengi.
Wanafunzi hao wanatoka katika vyuo vifuatavyo; Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo cha Mipango, Chuo Kikuu cha Mtakatifu John, Chuo cha Tamisemi Hombolo, Chuo cha Ualimu cha Capital na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).
“Wateja wetu wengi ni kina dada hasa wa vyuo vikuu ila wanaume wanakuja baadhi kuosha miguu,” anasema.
Anasema biashara hiyo imeweza kumsaidia kuendesha maisha tofauti na ile ya mwanzo aliyokuwa akifanya ya kupiga picha.
“Zamani nilikuwa napiga picha, maisha yalikuwa kidogo magumu kwa sababu ilikuwa mpaka nisafishe ndio nipeleke kwa mteja tofauti na biashara ya kucha ambapo ukimaliza unapewa chako hapo hapo,” anasema.
Kwa upande wake Thabit Rajabu, anasema alianza biashara hiyo miaka sita iliyopita huku kazi yake kubwa ikiwa ni kubandika kucha.
“Nabandika kucha za kila aina, kuna fupi na ndefu… wateja wangu ni wanafunzi. Hapa huwa sikai sana kutokana na kupigiwa simu niwafuate huko vyuoni.
“Simu yangu ndio ofisi wateja wangu ni wanafunzi hivyo wanapeana namba zangu,” anasema Rajabu.
Anasema kupitia kazi yake hiyo ameweza kujenga nyumba pamoja na kutatua kero mbalimbali za fedha katika familia yake.
“Nyerere Square ni eneo muhimu kwetu na maisha yetu yanakwamuka kimaisha kupitia eneo hili, wakati mwingine unasema asante Mungu kwa kipaji hiki,” anasema.
Changamoto
Richard Babisha anasema changamoto kubwa wanayokutana nayo ni wanawake kuacha wazi baadhi ya maumbile yao kama vile mapaja hivyo kuwa na wakati mgumu pindi wanapowahudumia.
“Wanawake wanaokuja hapa ni wazuri nadhani na wewe unawaona, sasa wakati wa kumpaka rangi unaweza kukuta kavaa kimini halafu miguu anaiweka kwenye mapaja yako.
Post a Comment