0
Kwa akali watu 38 wameuawa na wengine 86 kujeruhiwa katika mashambulizi pacha ya mabomu ya kutegwa kwenye magari katika mji wa Samawa, kusini mwa Iraq.

Polisi ya Iraq imesema kuwa, shambulizi la kwanza limefanyika karibu na ofisi ya serikali, huku la pili likifuata dakika chache baadaye katika kituo cha mabasi mjini Samawa.

Kituo cha Afya cha Muthanna katika mji huo kimewaambia waandishi wa habari kuwa, yumkini idadi ya walioaga dunia kutokana na hujuma hiyo ya kigaidi ikaongezeka kutokana na majeraha mabaya waliyopata waliokimbizwa katika hospitali za mji huo.

Mji wa Samawa ambao aghalabu ya wakazi wake ni Waislamu wa madheheu ya Shia unapatikana yapata kilomita 370 kusini mwa mji mkuu, Baghdad. Tarayi kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh limekiri kuhusika na mashambulizi hayo ya leo.

Hapo jana, wafanyaziara 24 waliuawa shahidi na makumi ya wengine kujeruhiwa kufuatia mlipuko wa bomu la kutegwa garini uliotokea katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad. Vyombo vya usalama vya Iraq vimesema kuwa, bomu hilo lilitegwa katika njia wanayopita wafanyaziara katika eneo la Nahrawan kusini mashariki mwa Baghdad.

Post a Comment

 
Top