JESHI la Magereza hapa nchini limesema kinara wa kuuza dawa za
kulevya, Ali Khatib Haji maarufu kwa jina la Shikuba amekuwa tishio
katika Gereza la Lindi.
Akitoa changamoto za magereza Dar es Salaam jana kwa Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi na Dawa za Kulevya, Kamishna Jenerali wa
Magereza, John Minja, alisema kutokana na hali hiyo wamelazimika
kuongeza ulinzi kwa kuwa miundombinu ya gereza hilo ambako Shikuba
anashikiliwa ni hafifu.
Minja alivitaka vyombo vinavyoshughulikia kesi hiyo kuharakisha
upelelezi ili Shikuba aliyekamatwa mwaka 2014 katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) baada ya kusakwa kwa zaidi ya miaka
miwili na polisi kutokana na tuhuma za dawa za kulevya huku akidaiwa
kuwa na mtandao mkubwa Afrika Mashariki, China, Brazil, Canada, Japan,
Marekani na Uingereza apelekwe mahakamani.
“Jeshi la Magereza limekuwa na changamoto ya uhaba wa fedha za
kufanya ukarabati na upanuzi wa magereza ya zamani ili yawe na
miundombinu inayoendana na ongezeko la wafungwa na mahabusu, mfano
unapokuwa na mtu kama Shikuba yule ni mtu hatari hata Marekani
wanamtafuta na imetulazimu kuongeza ulinzi katika Gereza la Lindi
ambako yupo mahabusu. “Naomba vile vyombo vinavyohusika na kesi yake
viweze kuharakisha upelelezi wa kesi ili apelekwe mahakamani,” alisema
Minja.
Pia alitoa mfano wa Gereza la Biharamulo lililopo mkoani Kagera
ambalo alisema lilijengwa mwaka 1897 na tangu kipindi hicho halijawahi
kufanyiwa ukarabati.
Minja alitoa mfano mwingine wa Gereza la Keko lililopo Dar es Salaam
na alisema lilijengwa mwaka 1959 likiwa na uwezo wa kuingiza wafungwa
340 lakini sasa hivi lina wafungwa 1,200.
Awali, hoja ya Shikuba ambaye hivi karibuni Marekani ilitangaza
kutaifisha mali zake zilizotokana na faida haramu ya biashara zake za
kuuza dawa hizo iliibuliwa katika kamati hiyo na Mbunge wa Singida
Magharibi (CCM), Elibariki Kingu.
Mbunge huyo alishangaa kesi ya Shikuba kucheleweshwa kufikishwa
mahakamani ikiwa ni mwaka wa tano tangu dawa za kulevya anazohusishwa
nazo kukamatwa.
“Lazima DPP (Mkurugenzi wa Mashtaka) aamshwe. Haiwezekani upelelezi
unafanyika kwa miaka mitano mtu hafikishwi mahakamani, Shikuba
amekamatwa muda mrefu sasa tunataka tuambiwe ni lini atafikishwa
mahakamani na mimi katika hili siogopi nipo tayari kufa lakini najua
siwezi kufa hadi nikamilishe kazi aliyonituma Mungu,” alisema Kingu.
Akitolea ufafanuzi suala hilo, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP),
Ernest Mangu, alisema Shikuba alikamatwa miaka miwili baada ya dawa
hizo kukamatwa na licha ya kutajwa na wale waliokamatwa mwenyewe
hakukubali kwamba anahusika.
“Hii kesi inahitaji uchunguzi hatuwezi kusema kwa sababu ametajwa
basi na yeye atakubali. Tulimkamata Februari, 2014 na alikana hivyo
lazima tuchunguze na tuweze kuthibitisha,” alisema Mangu.
Aliwapa matumaini wabunge kuwa jeshi hilo lipo kwenye hatua nzuri ya kukamilisha upelelezi na watampeleka mahakamani.
“Tuko katika hatua nzuri ya kukamilisha upelelezi na atapelekwa mahakamani siku za hivi karibuni,” alisema Mangu.
Post a Comment