*Yumo bosi wa zamani wa TRA na Miss Tanzania wa zamani
*Mbunge Ndassa naye aunganishwa tuhuma za rushwa
KAMISHINA Mkuu wa zamani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry
Kitilya, aliyekuwa Ofisa Mwandamizi wa Benki ya Stanbic tawi la
Tanzania, Shose Sinare na aliyekuwa Mwanasheria wa benki hiyo, Sioi
Solomon, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
wakikabiliwa na mashitaka nane.
Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo jana na Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wakikabiliwa na mashitaka hayo,
yakiwamo ya kula njama, kughushi kujipatia fedha kwa njia ya
udanganyifu na utakatishaji wa dola milioni sita za Marekani, sawa na
zaidi ya Sh bilioni 12 ambazo ni mali ya Serikali ya Tanzania.
Washitakiwa hao walipandishwa kizimbani hapo kutokana na tuhuma za
ufisadi zilizowahi kuibuka baada ya Serikali ya Tanzania kudaiwa
kupoteza zaidi ya Sh trilioni 1.3 katika kipindi cha kati ya mwaka 2012
na 2013, wakati ikiuza hati fungani zake kwa Benki ya Stanbic
inayomilikiwa na Standard Group ya Afrika Kusini.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Emilius Mchauru, Wakili wa Serikali Mkuu,
Oswald Tibabyekomya kwa kushirikiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi,
Christopher Msigwa, waliwasomea washitakiwa mashitaka hayo.
Katika shitaka la kwanza, washitakiwa hao katika tarehe tofauti kati
ya Agosti, 2012 na Machi, 2013 ndani ya Jiji la Dar es Salaam, walikula
njama ya kutenda kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Shitaka la pili hadi la tano yanamkabili Shose peke yake, aliyewahi
kuwa mrembo wa Tanzania mwaka 1996, ambapo ilidaiwa kwamba Agosti 2,
2012 akiwa katika makao makuu ya benki hiyo yaliyopo Dar es Salaam, kwa
nia ya kudanganya alighushi hati ya mapendekezo ya uwezeshwaji wa
kifedha ya Agosti 2, 2012 kwa lengo la kuonyesha kuwa benki hiyo kwa
kushirikiana na Benki ya Standard ya Uingereza watatoa mkopo wa dola
milioni 550 za Marekani kwa Serikali ya Tanzania kwa ada ya asilimia 2.4
ya mkopo huo wakati akijua si kweli.
Mshitakiwa huyo pia anadaiwa kwamba Agosti 13, 2012 katika ofisi za Wizara ya Fedha aliwasilisha hati hiyo.
Shose pia anadaiwa kwamba Septemba 20, 2012, akiwa katika makao makuu
ya benki hiyo yaliyopo Wilaya ya Kinondoni, alighushi barua ya
pendekezo la mkopo huo ya Septemba 20, 2013, akionyesha kwamba Benki ya
Standard Plc kwa kushirikiana na Benki ya Stanbic tawi la Tanzania
wangetoa mkopo huo kwa Serikali kama benki hizo zitapewa kazi ya
kutafuta mkopo huo kwa riba ya asilimia 2.4, wakati akijua si kweli.
Mshitakiwa huyo pia anadaiwa kuwasilisha nyaraka hiyo ya kughushi katika Wizara ya Fedha.
Shitaka la sita linawakabili washitakiwa wote ambapo wanadaiwa kuwa
Novemba 5, 2012, wakiwa katika makao makuu hayo kwa nia ya kudanganya
walighushi mkataba wa ushirikiano wa tarehe hiyo kwamba Benki ya Stanbic
Tanzania Limited imeanzisha ushirikiano na Kampuni ya Enterprise Growth
Market Advisors (EGMA) Limited kwa ajili ya kutafuta mkopo huo kwa
Serikali.
Ilidaiwa kwamba Egma pia ingewezesha na kuandaa mikutano na nyaraka
mbalimbali ambazo zingetakiwa na mamlaka za Tanzania wakati wakijua si
kweli.
Katika shitaka la saba, washitakiwa hao wanadaiwa kwamba katika
tarehe tofauti Machi 2013, ndani ya Dar es Salaam kwa udanganyifu
walijipatia dola milioni sita kutoka serikalini kwa kudanganya kwamba
fedha hizo ni ada ya malipo kwa Egma na Benki ya Stanbic tawi la
Tanzania kwa kuwezesha Serikali kupata mkopo wa dola milioni 600 za
Marekani.
Pia washitakiwa wote wanadaiwa kutakatisha kiasi hicho cha fedha kwa
kuzihamisha katika akaunti mbalimbali, ikiwemo zenye namba
0240026633702, 0240026633701 na 9120001251935 zinazomilikiwa na Egma
katika Benki ya Stanbic tawi la Tanzania na akaunti namba 3300605539 na
3300603692 ambazo pia zinamilikiwa na Egma katika Benki ya KBC, wakati
wakijua fedha hizo si za Egma bali ni zao.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo, wote waliyakana na upande wa mashitaka ulidai kutokamilisha upelelezi.
Hata hivyo, kulizuka mabishano ya kisheria kuhusu dhamana ya
washitakiwa hao, ambapo upande wa utetezi ukiwakilishwa na Wakili Dk.
Ringo Tenga, alitaka washitakiwa hao wapate dhamana, huku upande wa
mashitaka ukipinga kwa madai ya kwamba shitaka la utakatishaji fedha
halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Kutokana na mabishano hayo, hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili
8, mwaka huu, atakapotoa uamuzi. Washitakiwa wote wamerudishwa rumande
hadi tarehe hiyo.
NDASSA KORTINI
Kabla ya kina Kitilya kufikishwa, Takukuru ilimburuta mahakamani hapo
Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa (56), kwa tuhuma ya kuomba rushwa
ya Sh milioni 30 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO), Mhandisi Felchesmi Mramba.
Ndassa, aliyefikishwa kortini hapo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,
Emmilius Mchauru, anakuwa mbunge wa nne kufikishwa mahakamani hapo baada
ya wenzake watatu wa CCM (Kangi Lugola wa Mwibara, Sadiq Murad wa
Mvomero na Victor Mwambalaswa wa Lupa), wakiwa ni wajumbe wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC) kufikishwa juzi kwa tuhuma
za kuomba rushwa ya Sh milioni 30 kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Manispaa ya Gairo, Mbwana Magotta, ili wamsaidie kutoa mapendekezo
mazuri ya taarifa ya hesabu za halmashauri hiyo za mwaka 2015/2016.
Wakili wa Serikali kutoka Takukuru, Dennis Lekayo, alimsomea Ndassa
mashtaka hayo mawili ya kujihusisha na vitendo vya rushwa anayodaiwa
kuyatenda Machi 13, mwaka huu, jijini Dar es Salaam.
Lekayo alidai siku hiyo, Ndassa akiwa mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Uwekezaji, alijihusisha na vitendo vya rushwa kwa kushawishi
kupewa Sh milioni 30 kutoka kwa Mramba, ikiwa ni ushawishi kwa wajumbe
wenzake wa kamati hiyo ili kutoa mapendekezo mazuri kwa Tanesco katika
ripoti yao ya hesabu kwa mwaka 2015/2016.
Pia Ndassa anadaiwa siku hiyo katika jiji hilo akiwa mbunge na mjumbe
wa kamati hiyo, alijihusisha na vitendo vya rushwa kwa kushawishi
kupatiwa huduma ya umeme kutoka kwa Mramba kwa kumpatia mdogo wake,
Matanga Mbushi na rafiki yake, Lameck Mahewa kama faida ili awashawishi
wajumbe wenzake wa kamati hiyo watoe mapendekezo mazuri katika hesabu za
Tanesco za mwaka huo wa fedha.
Mshitakiwa huyo anayewakilishwa na Wakili Erasto Lugenge kwa niaba ya
Wakili Aloyce Mandebebe, alikana shitaka hilo na upande wa Jamhuri
ulidai upelelezi haujakamilika na kuomba shauri hilo kuahirishwa hadi
tarehe nyingine kwa kutajwa.
Pia Lekayo aliomba mahakama kutoa masharti magumu ya dhamana kama
itakavyoona inafaa, akihofu kuwa kutokana na nafasi ya mshitakiwa katika
jamii, anaweza kuingilia uchunguzi.
Upande wa utetezi ulidai hawaoni sababu za mshitakiwa kupewa masharti
magumu kwa kuwa upande wa Jamhuri haujaeleza namna anavyoweza kuingilia
upelelezi.
Hakimu Mchauru alitoa masharti ya dhamana yaliyomtaka Ndassa kutia
saini dhamana ya Sh milioni 10 na kuwa na mdhamini mmoja wa kuaminika
ambaye naye atatia saini kiasi hicho cha fedha.
Ndassa alitimiza masharti hayo na aliachiwa kwa dhamana hadi Aprili 18, mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa tena.
Baada ya kuachiwa kwa dhamana, Ndassa akiwa anajiandaa kutoka katika
viwanja vya mahakama hiyo alisema: “Hivi mbunge akiomba nguzo kwa ajili
ya wapigakura wake ili Tanesco iweze kupata mapato ni kosa.”
Kitendo cha wabunge hao kufikishwa mahakamani kwa siku mbili
mfululizo kimekuja baada ya gazeti hili kuripoti hivi karibuni kuwa kuna
baadhi ya wabunge waliomba rushwa katika taasisi za Serikali na Machi
22, mwaka huu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alifanya mabadiliko ya baadhi
ya wajumbe wa Kamati za Bunge, kisha akawapangua wenyeviti na makamu
wenyeviti watano wa kamati walizoziongoza
Post a Comment