Magufuli: Majipu yakinishinda bora niache urais
RAIS Dk. John Magufuli, amesema kama atashindwa kutumbua majipu dhidi ya wazembe na wabadhirifu serikalini, hana sababu ya kuendelea kushika wadhifa huo.
Amesema endapo hali hiyo ikitokea ni bora arudi nyumbani kwake akalale, kwa sababu lengo lake la kuwapatia wananchi Tanzania mpya, litakuwa halijatimia.
Rais Dk. Magufuli aliyasema hayo jana, wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Arusha-Holili yenye urefu wa kilometa 234.3, itakayogharimu Sh bilioni 209.3
“Ndugu zangu kazi hii ni ngumu, wapo watu ambao hawataki mimi na Serikali yangu kuwatumbua, nitapambana hadi nihakikishe ninafanikiwa.
“Na iwapo nitashindwa hakuna sababu ya mimi kuendelea kuwa Rais wa nchi hii, ni bora nirudi nyumbani kwangu kulala,” alisema.
Dk. Magufuli alisema amejitoa sadaka kwa ajili ya Watanzania na hivyo amewakumbusha wananchi waendelee kumwombea kwa Mungu, ili akamilishe kazi hiyo ngumu.
Alisema amekuwa akipata vikwazo wakati wa kutumbua majipu, katika hatua mbalimbali anazochukua dhidi ya watumishi wa umma wanaotumia vibaya madaraka yao.
“Tanzania ilikuwa imegeuka kuwa shamba la bibi, ilikuwa nchi ya ovyo kweli kweli, nimejitosa kuwa sadaka ya Watanzania, nihakikishe kuwa nitawavusha kutoka katika lindi kubwa la umasikini linalowakabili wananchi wa pato la chini,” alisema.
Rais Dk. Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), amewataka wakuu wenzake wa nchi wananchama wa jumuiya hiyo kuhakikisha wanatimiza wajibu waliokabidhiwa na wananchi ili kuwasaidia kutoka kwenye umasikini.
Alisema umefika wakati viongozi wa nchi wanachama kuamka na kufanya kazi kwa bidii kwa lengo la kuwanufaisha wanachi wao ambao wengi wanateseka na umasikini, wakati nchi zao zimejaliwa rasilimali nyingi ikiwemo madini, mbuga za wanyama, gesi asilia, mafuta,misitu na ardhi nzuri kwa ajili ya kilimo.
Alisema barabara hiyo ikikamilika, itaharakisha maendeleo ya wananchi wa nchi wanachama katika nyanja za kilimo, biashara, viwanda na usafirishaji.
“Tutakapokamilisha barabara hii, tutaendelea na ujenzi wa barabara zitakazounganisha nchi zote za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, tuunganishe Tanzania na Rwanda na Burundi, tuunganishe Tanzania na Uganda na hatimaye mtandao wa barabara uziunganishe nchi zote sita” alisema Rais Dk.Magufuli.
Alisema kati ya fedha hizo, Sh bilioni 190 zimetolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), huku kiasi cha Sh bilioni 19.4 zikitolewa kwa pamoja kati ya Serikali ya Tanzania na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.
Post a Comment