Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Taifa, Shaka Hamduni
Shaka amewataka wanachama wanaojitambua kuwa ni majipu kwa kukisaliti
chama kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka jana, waanze kujitumbua kabla
hawajatumbuliwa.
Shaka alitoa rai hiyo jana katika mji wa Orkesumet na Kata ya Ngorika
Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara wakati wa ziara yake ya kuhamasisha
vijana kujiunga na chama hicho, kufungua matawi mapya, kumsimika kamanda
wa Kata ya Naisinyai na kukagua uhai wa chama.
Alisema lazima wajenge chama chenye heshima na nidhamu kuliko kuwa na wanachama wasaliti ambao hawana msimamo.
Shaka alisema wanachama wa aina hiyo nyakati za asubuhi wanakuwa sehemu moja na ikifika jioni wanakwenda kwingine.
“Ni heri wabakie wanachama wawili waadilifu kuliko wengi ambao hawana
msimamo, kufanya kosa siyo kosa, bali kosa kurudia kosa, tunajua
uchaguzi ukirudiwa tena hapa Simanjiro CCM itafanikiwa kushinda,”
alisema Shaka.
Alisema kukata tamaa ni mwiko ukiwa CCM, kwa kuwa miaka mitano siyo
mingi, hivyo wanatarajia kurudisha kata sita na Jimbo la Simanjiro
linaloshikiliwa na Chadema.
Alisema hilo litafanikiwa kutokana na uongozi bora wa Rais John Mafuguli.
“Tumesikia wapo waliotusaliti wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita,
tutawachukulia hatua, ila hivi sasa kutokana na juhudi za Rais Magufuli
hata upinzani watatupigia kura za ndiyo,” alisema.
Mwenyekiti wa UVCCM, Wilayani Simanjiro, Kiria Laizer alisema vijana
ndiyo nguvu ya chama, hivyo kupitia jumuiya hiyo wamejipanga kukipigania
na kukitetea.
“Vijana ndiyo nguzo ya chama, tumejipanga vizuri kuhakikisha kupitia
CCM, wananchi wa eneo hili wanaendelea kukiamini na kukithamini, hivyo
tutasonga mbele,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment