0
Baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutangaza operesheni ya kuwaondoa ombaomba katikati ya jiji, ombaomba hao wameendelea kuviziana na askari mgambo huku wakidai wanaangalia upepo unavyokwenda.

Kazi ya kuwakamata ombaomba hao inafanywa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala.

Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Isaya Mngurumi alisema kazi hiyo inaendelea huku baadhi yao wakiwa wamefikishwa mahakamani. “Kazi hii ni endelevu, ombaomba walikuwa kero katikati ya jiji letu, hivyo tutahakikisha wote wanakamatwa,” alisema Mngurumi.

Gazeti hili lilitembelea maeneo ya katikati ya jiji ikiwamo barabara ya Bibi Titi na kushuhudia ombaomba hao wakiomba fedha kwa wapita njia na kwenye magari.

Mmoja wa ombaomba hao, Abdallah Isaya alisema wanalazimika kuomba kutokana na ulemavu walio nao.

Alisema wanaomba kwa kuvizia kwa kuhofia kukamatwa na mgambo na pale wanapotokea hupanda baiskeli zao na kuondoka. Baadhi ya ombaomba walisema wanaishi maisha magumu na kulazimika kuomba fedha kwenye magari yanayosiamama pembezoni mwa barabara. “Juzi wenzetu walikamatwa na mgambo sisi tulikimbia na kwenda kujificha,” alisema mmoja wao.

Kamanda wa Polisi Ilala, Lucas Mkondya alisema operesheni ya kuwakamata inafanywa na jiji kama wakishindwa jeshi hilo litawasaidia.

Post a Comment

 
Top