Kambi ya Upinzani bungeni jana imesusia kuwasilisha na kujadili hotuba
ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, huku
kiongozi wake, Freeman Mbowe akitoka nje ya ukumbi huo, akitaja kasoro
tatu zilizosababisha wachukue uamuzi huo.
Staili ya kususia kujadili hotuba hiyo ya bajeti ni mpya kwa kambi hiyo
ya upinzani baada ya kutumia njia ya kutoka nje ya ukumbi wakati wa
vikao vya Bunge la Katiba na baadaye kutumia njia ya kupiga kelele
kukwamisha shughuli za chombo hicho wakati wa Bunge la Kumi.
Jana, Mbowe aliwaambia waandishi nje ya ukumbi kuwa kasoro zilizofanya
wachukue uamuzi huo ni kukiuka masuala ya kisheria katika utekelezaji wa
bajeti, kutotangaza kwenye Gazeti la Serikali mabadiliko ya wizara na
kutorushwa kwa vipindi vya Bunge kwenye televisheni.
Mbowe, ambaye alikuwa akitarajiwa kusoma bajeti ya upinzani kuhusu Ofisi
ya Waziri Mkuu, aliibuka na hoja hizo tatu kabla ya kuamua kutoka nje.
“Bajeti inakuwapo kwa sababu ni hitaji la kisheria. Inapokuwa Serikali
inataka kupitisha bajeti, lakini haiheshimu bajeti hakuna sababu ya
wabunge kukaa hapa kujadiliana, kutoa povu, kupitisha vifungu vya
Katiba, halafu yenyewe haitekelezi wajibu wake kisheria,” alisema Mbowe
nje ya ukumbi wa Bunge.
Alisema Serikali imekuwa ikikiuka sheria ya utekelezaji wa majukumu ya
mawaziri inayomtaka Rais kutengeneza mwongozo wa muundo wa utekelezaji
wa majukumu ya Serikali yake, ikiwa ni pamoja na kutangaza katika gazeti
la Serikali mabadiliko ya wizara zake.
Alisema “Tulichelewa kuunda (Baraza Kivuli la Mawaziri) kwa sababu
tulikosa instrument (nyaraka rasmi). Tukalazimika kuunda hivyohivyo.
Sasa tumefika kwenye (Bunge bado Serikali haijaundwa officially (rasmi),
kisheria. Haijawa gazetted (haijatangazwa kwenye Gazeti la Serikali),”
alisema Mbowe.
“Mpaka leo Serikali hii inafanya kazi kwa kutumia instrument
iliyosainiwa na Rais (wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya) Kikwete mwezi
wa 12 mwaka 2010.
“Na wizara kuu kwa mujibu wa instrument ya mwaka 2010 ilikuwa ni Wizara
ya Waziri Mkuu Tamisemi. Na Tamisemi ilikuwa chini ya Ofisi ya Waziri
Mkuu. Kwa hiyo baada ya uchaguzi wa 2010, Tamisemi imerudishwa Ofisi ya
Rais, haiku tena Ofisi ya Waziri Mkuu. Lakini haijawa gazetted.”
Alitaja hoja nyingine kuwa ni uvunjwaji wa Katiba na sheria za nchi
kuhusiana na bajeti unaofanywa na Serikali pamoja na kuminya uhuru na
madaraka ya mhimili wa Bunge kwa kuzuia matangazo ya wasusia Bunge
kurushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni.
“Hatutashiriki mjadala tunaendelea kutafakari hatua nyingine za kuchukua
kama Serikali na Bunge hawatatafuta ufumbuzi wa masuala hayo matatu,”
alisema Mbowe.
Mbowe aliingia ukumbini saa 9:56 alasiri akiongozana na mbunge wa Momba,
David Silinde na alikwenda kusalimiana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali
(AG) George Masaju na Waziri wa Kilimo, Mwigulu Nchemba.
Mara baada ya kupewa nafasi na Mwenyekiti wa Bunge Andrew Chenge, Mbowe
alieleza sheria ya utekelezaji wa majukumu ya mawaziri ambapo alidai
kifungu cha 5(1) kinaweka masharti kwa Rais kutengeneza mwongozo wa
muundo na utekelezaji wa majukumu yake.
Alisema mpaka sasa Serikali inafanya kazi bila kuwa na mwongozo wa
utendaji kwa wizara mbalimbali hivyo kazi nyingi za Serikali zinafanywa
kwa kauli ya Rais.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo mpaka sasa mwongozo wa utendaji wa Serikali
kwa kila wizara unaotumika ni uliochapishwa kwenye Gazeti la Serikali
Namba 494 A la Desemba 17, 2010 ambao pia umetoa majukumu ya Ofisi ya
Waziri Mkuu.
Kiongozi huyo alinukuu baadhi ya majukumu katika mwongozo huo kuwa ni
kuratibu shughuli za Serikali, kiongozi wa Serikali ndani ya Bunge,
kiungo kati ya Bunge na Serikali, shughuli za kisiasa na serikali na
kuratibu sherehe na misaada mbalimbali.
“Kazi nyingine ni kusaidia urahisishaji wa mipango ya serikali katika
kuhamishia makao makuu Dodoma, uwekezaji, uchumi, sekta binafsi na
kusaidia maendeleo katika sekta za ndani,” alisema Mbowe.
Alisema Rais John Magufuli alifanya mabadiliko ya kuziunganisha wizara bila kubadili muongozo wa kisheria.
“Kitendo cha Serikali hii kuendesha kazi zake kwa mwongozo wa 2010 kina
maana kwamba majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu bado ni yale yale ya mwaka
2010 kwa sababu gazeti hilo halijafutwa,” alisema.
Alifafanua kuwa jambo hilo ni uvunjwaji wa Katiba na sheria za nchi
kuhusu bajeti unaofanywa na serikali na kwa mujibu wa Ibara ya 63 (3)
(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bunge limepewa mamlaka
ya kujadili utekelezaji wa kila wizara na kuidhinisha bajeti ya
Serikali.
Mbowe alisema ikiwa fedha zilizoidhinishwa na bunge hazikutosha
kutekeleza majukumu, kifungu cha 41 (1) cha Sheria ya Bajeti ya mwaka
2015 kinaelekeza kuwa serikali itawasilisha bungeni maombi ya idhini,
bajeti ya nyongeza ya fedha zilizotumika ambazo zimezidi kiwango.
Alituhumu kuwa kumekuwa na uvunjwaji wa kifungu hicho na kutolea mfano
bajeti ya Wizara ya Uchukuzi na Mawasiliano ya mwaka wa 2015/16 ilikuwa
Sh 883.8 bilioni ambazo kati ya hizo, fedha za ndani zilikuwa Sh191.6
bilioni.
“Jambo la kushangaza ni kwamba hadi kufikia mwezi Machi 2016 Wizara
ilikuwa imeshapokea kutoka hazina Sh607.4 bilioni ikiwa ni fedha za
ndani, kitendo kinachoonyesha kuwa na ongezeko kubwa la fedha za ndani,”
alisema.
Alitaja kuwa tangu kuidhinishwa kwa bajeti ya Wizara ya Ujenzi, hakuna
bajeti ya nyongeza iliyopelekwa bungeni na Serikali kwa ajili ya kupata
idhini kutokana na matakwa ya Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015 au sheria
ya fedha ya 2015.
“Kitendo cha Serikali kuamua kuhamisha kiasi cha fedha ya bajeti bila
ya kupata idhini ya Bunge ni dharau kwa bunge lakini mbaya zaidi ni
uvunjwaji wa Katiba na sheria.” alisema.
Nje ya ukumbi wa Bunge alisema:”Ukiwauliza wanapata wapi hizi fedha,
wanasema ni maelekezo ya Rais kwamba fedha ziondolewe kwenye fungu hili,
zipelekwe wizara hii.”
Vipindi vya Bunge
Kadhalika, Mbowe alisema uamuzi wa Serikali kuminya uhuru na madaraka
ya Bunge umewapora wananchi haki yao ya kupata habari kwa kuzuia
mijadala bungeni kurushwa moja kwa moja na vyombo vya habari.
Alisema jambo hilo ni uvunjwaji wa Ibara ya 18 ya Katiba inayotoa uhuru
kwa kila mtu kutoa maoni na kueleza fikra zake, kutafuta, kupokea na
kutoa habari.
“Bunge ndipo mahali ambapo wananchi wanahoji na kuiwajibisha Serikali na
wanajadili hoja za maendeleo kupitia wabunge wao waliowachagua, hivyo
huwafuatilia kupitia kwenye luninga zao pia ubadhirifu wa miradi mingi
uibuliwa huko,” alisema.
Alisema wapinzani wataendelea kutafakari kwa kina na makini hatua za kufuata na kisha akawasilisha.
“Kwa mazingira kama hayo, kambi rasmi ya upinzani bungeni haiko tayari
kuendelea kushiriki katika uvunjaji Katiba, sheria na haki za msingi za
wananchi,” alisema.
“Kambi rasmi haitakuwa tayari kuwasilisha hotuba yake katika mazingira
haya na inaushauri uongozi wa Bunge kutafuta ufumbuzi wa haraka wa
kadhia hii ili kurejesha heshima ya Bunge na haki za msingi.”
Baadaye, Chenge aliipinga kauli ya Mbowe kuwa Katiba imevunjwa na kusema
alitumia maneno mazito na badala yake alimtaka atumie maneno kuwa
Katiba ilitaka kuvunjwa.
Chenge aliitaka kambi ya upinzani kufuata taratibu kama wanaona kuwa
wameonewa, badala ya kutumia maneno hayo na pia akata watafakari kama
wangependa kuendelea na mjadala.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge wa upinzani walionyesha kususia kwani hata
walipoitwa na mwenyekiti hawakuchangia licha ya kuwapo ndani ya ukumbi
wa Bunge.
Kauli ya Mbowe kwa wanahabari
Akizungumza na wanahabari Mbowe alisema uamuzi huo haujakiuka sheria kwa
sababu Bunge liko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na kwamba hawawezi
kwenda mahakamani ili kupata tafsiri kuhusu suala hilo kwa sababu
shughuli za Bunge zinatatuliwa na Bunge lenyewe si mahakama.
“Rais kama kiongozi wa nchi ana mamlaka ya kulisemea hili, atueleze kama
ni yeye ndiye aliyeruhusu Bunge lisirushwe moja kwa moja. Awali
walisema TBC hawatarusha ila kwa sasa vyombo vyote vimezuiwa,” alisema.
“Hivi sasa luninga zilizopo ndani ya Bunge zilizokuwa zikionyesha
matangazo nazo hazionyeshi kinachoendelea. Sasa watumishi wa Bunge
watafuatilia nini?” alihoji Mbowe.
Kauli ya AG
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George
Masaju alisema: “Nitashukuru kama mtavuta subira majibu ya Serikali
yatatolewa wakati wa kufanya majumuisho.”
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment