0
  
 
dk.slaa

WAKATI machungu ya nchi 10 wahisani na Shirika la Marekani la Changamoto za Milenia (MCC) kukataa kuchangia bajeti ya taifa na kutoa misaada yakiwa bado hayajaisha, inadaiwa Tanzania iko hatarini kuingizwa kwenye orodha mpya ya nchi zisizo salama kiuwekezaji.

Mpango wa kuingiza Tanzania katika kundi hilo la mataifa ambayo mazingira ya uwekezaji si salama “Risky investment destination” unadaiwa kuratibiwa na mashirika makubwa ya fedha ya Marekani na Ulaya.

Iwapo hilo litatokea, hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania katika kipindi cha zaidi ya miaka 10 iliyopita, kuondoka katika orodha ya mataifa yanayoendelea duniani ambayo yamekuwa yana mazingira mazuri ya kuvuta mitaji ya uwekezaji kutoka mataifa yaliyoendelea.

Katika hilo, inaelezwa pia kuwa uamuzi huo utaathiri utendaji na ufanisi katika sekta binafsi sambamba na kugusa na pengine kuzikwamisha taasisi za kimataifa ambazo zilikuwa zije nchini kwa shughuli za kiuwekezaji.

Miongoni mwa taasisi ambazo zinaweza kuguswa na uamuzi huo ni zile za Ulaya na Marekani ambazo zinajihusisha na utafiti wa gesi na mafuta hapa nchini.

Akizungumza na Mtanzania Jumapili katika mahojiano maalum kutoka Canada anakoishi, mwanasiasa na Katibu Mkuu wa zamani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbrod Slaa alikiri kupata taarifa za kuwapo kwa mpango huo.

Akifafanua, Dk Slaa alisema anaamini iwapo uamuzi huo utatekelezwa unaweza kuwa na athari kubwa katika mipango ya maendeleo kutokana na kuongeza nakisi katika Bajeti ya Serikali.

Mwanasiasa huyo ambaye anayo rekodi ya kunasa taarifa kadhaa za kitaifa na kimataifa kuhusu mwenendo wa masuala yanayohusu siasa, demokrasia na utawala bora alisema, athari za uamuzi huo iwapo utatekelezwa zinaweza kuwa ni kubwa kuliko zile za MCC na mataifa 10 yaliyosusia kuchangia bajeti ya Tanzania.
Dk. Slaa, alisema pamoja na kwamba hakuna kikwazo rasmi cha kiuchumi ambacho kitawekwa kwa Tanzania, mashirika ya nje kama ya utafutaji wa mafuta, gesi, uranium na madini yote kwa ujumla, yatashindwa kufanya kazi kwa kukosa fedha kutokana na masharti magumu ya kupata fedha hizo tofauti na ilivyo sasa.
“Mwenendo wa biashara na sekta ya utalii vinaweza kudorora hatimaye kuwa ghali sana,” alisema Dk. Slaa.
Dk. Slaa alisema iwapo uamuzi huo utachukuliwa utakuwa ni wa kwanza na mgumu katika historia kwa mashirika ya fedha ya Marekani na Ulaya dhidi ya Tanzania.
Akizungumzia hatua ya MCC kuifutia misaada Tanzania na pia nchi 10 wahisani kukataa kuchangia bajeti kuu ya Serikali, alisema pamoja na kwamba uamuzi huo utaathiri taifa, unapaswa kuchukuliwa kama somo muhimu la kututaka kuacha utegemezi na hulka ya kuombaomba.
“Ni kweli uamuzi wa kukosa mabilioni ya fedha kutoka kwa wahisani mbalimbali wa Marekani na wa Ulaya unaweza kuwa na athari kubwa katika mipango yetu kwa kuwa kutatokea pengo katika bajeti yetu,” alisema.
Hata hivyo, Dk. Slaa alitolea mfano nchi ya Afrika Kusini wakati wa ubaguzi wa rangi, akisema si tu ilinyimwa misaada bali iliwekewa vikwazo vya kiuchumi, lakini walifunga mikanda.

Akifafanua Dk. Slaa alisisitiza kuwa Tanzania haitafikia hatua ya kujitegemea kiuchum
i kama ilivyo Afrika Kusini leo iwapo kila wakati itapaswa kupiga magoti kwa wahisani.

Akiwazungumzia wahisani ambao sasa wamesitisha misaada, Dk Slaa alisema; “Wao pia wanahitaji ‘resources’ (raslimali) tulizonazo, ni suala la muda tu. Watarudi wenyewe bila kubembelezana.

Watakaporudi tutaheshimiana kwa kuwa wakati huo na sisi tutakuwa tumejenga uwezo wetu.
Mwanasiasa huyo alisema, wakati umefika kwa Tanzania kama taifa kuacha kuuza bidhaa ghafi katika soko la dunia na badala yake kuanza kuuza zile zilizotengenezwa katika viwanda kama njia ya kujenga uchumi madhubuti.

“Hii habari ya kuwauzia ‘raw materials’ (bidhaa ghafi) kisha ‘finished products’ zinarudi kwetu kwa bei ambayo asilimia 90 ya watu wetu (yaani wale waliozizalisha) hawawezi kununua bidhaa hizo, ni lazima ifike mahali tuseme basi. Inahitaji ‘bold decision’ (maamuzi magumu),” alisema Dk. Slaa.
Hivi karibuni MCC ilitangaza kuifutia msaada wa zaidi ya shilingi trilioni moja Tanzania, ikieleza kwamba Uchaguzi wa Zanzibar haukuzingatia demokrasia.

Mbali na suala la Zanzibar, MCC iliitaja pia Sheria ya Mitandao (Cyber Crime Act) kama inavunja misingi ya uhuru wa habari na kwamba mambo kama hayo hayaendani na misingi inayosimamia.
Uamuzi huo wa MCC uliungwa mkono siku chache baadae na nchi 10 wahisani ambazo zilitangaza kujitoa kuchangia bajeti kuu ya Serikali kwa sababu hizo hizo.

Dk. Slaa kwa upande wake alikataa kutoa maoni yoyote kuhusu hoja ya Zanzibar kutumiwa na MCC kama sababu ya kuondoa misaada yao.

 

Post a Comment

 
Top