SERIKALI imesema haitatoa kibali cha kuagiza mchele kutoka nje ya
nchi, lakini itaagiza kiasi kidogo cha sukari ili kufidia nakisi iliyopo
nchini hivi sasa kwa lengo la kuepusha mfumuko wa bei ya bidhaa hiyo
huku ikieleza kuwa baadhi ya wafanyabiashara wanaficha sukari ili
kusubiri bei ipande.
Aidha, imewaagiza maofisa biashara nchini kote kufanya ukaguzi katika
maduka ili kuhakikisha wafanyabiashara walioficha sukari ili kusubiri
bei kupanda wanaitoa sukari hiyo na kuiuza mara moja.
Hayo yalisemwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa akijibu hoja
za wabunge waliojadili hotuba ya Bajeti kwa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa
mwaka ujao wa fedha bungeni mjini hapa jana.
Akizungumzia sukari, Waziri Mkuu alisema kumejitokeza kwa upungufu
kidogo wa sukari nchini na serikali imeamua kuagiza kiasi hicho kutoka
nje ya nchi wakati ikiendelea kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa nchi
inapata uwezo wa kuzalisha kiwango cha sukari cha kutosha.
Alisema wakati nchi inahitaji tani 420,000 za sukari kwa mwaka, uwezo
wa viwanda vya ndani umekuwa ni tani 320,000 na hivyo kufanya kuwepo
kwa nakisi ya tani 100,000.
Alisema pamoja na mpango huo wa kuagiza sukari kutoka nje, serikali
itakuwa macho katika kuhakikisha kuwa sukari inayoruhusiwa kuingia ni
ile inayotakiwa na si zaidi, lengo likiwa ni kuvifanya viwanda vya ndani
kuendelea na uzalishaji hadi kuviwezesha kufikia uwezo wa juu wa
kukidhi mahitaji ya nchi.
Alisema pamoja na upungufu uliopo, serikali inazo taarifa kwamba
sukari iliyopo nchini hivi sasa inafikia tani 37,000, lakini baadhi ya
wafanyabiashara wamekuwa wakificha sukari waliyonayo ili kusubiri
kupanda kwa bei kutokana na upungufu uliopo.
“Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii kuwaagiza maofisa
biashara nchini kote wafanye ukaguzi ili kuhakikisha sukari haiachwi
ndani ili kusubiri bei kupanda. Ni lazima watoe sukari hiyo na wauze kwa
bei elekezi ya serikali,” alisema Waziri Mkuu na kuongeza: “Bei hiyo ya
serikali ndiyo itakayoruhusiwa kuwepo sokoni katika kipindi hiki cha
upungufu uliopo hadi pale sukari iliyoagizwa itakapoingia nchini
kutokana na kukamilika kwa taratibu zote za uagizaji wake.”
Hivi karibuni, Serikali ilitangaza kuwa bei elekezi ya sukari ni Sh
1,800 kwa kilo, lakini katika wiki za karibuni kumeibuka vilio vya
wananchi katika maeneo mbalimbali nchini kwamba bidhaa hiyo muhimu sasa
inauzwa kati ya Sh 2,200 hadi Sh 2,500 kwa kilo katika maeneo yao.
Kuhusu mchele, Waziri Mkuu alisema uzalishaji wa mpunga nchini
umeongezeka kwa asilimia 14 katika kipindi kinachoanzia mwaka 2009/2010
hadi mwaka 2014/2015, hatua iliyoifanya nchi kuwa na mchele wa kutosha.
Alisema kuongezeka kwa uzalishaji wa zao hilo kunatokana na jitihada
zinazoendelea kuchukuliwa na serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo
na Uvuvi katika kuhakikisha nchi inakuwa na hazina kubwa ya mazao ya
nafaka zaidi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment