0


kAFULILA-NA-HUSNA-MwilimaKESI namba mbili ya mwaka 2015 ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa Jimbo la Kigoma Kusini iliyofunguliwa na David Kafulila, jana imeshindwa kuendelea kusikilizwa kwa mara ya pili kutokana na mbunge wa jimbo hilo, Hasna Mwilima kushindwa kuhudhuria mahakamani.

Akielezea uamuzi wa kuhairishwa kwa kesi hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Kigoma, Sylvester Kainda, amesema Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Ferdinand Wambari, ameamua kuhairisha kesi hiyo kutokana na mlalamikiwa katika kesi hiyo kushindwa kufika mahakamani.

Kesi hiyo ilipangwa kuanza kusikilizwa mfululizo kuanzia Machi 9, mwaka huu lakini kutokana na Mwilima kushindwa kufika mahakamani, mahakama imeamua kuihairisha hadi Machi 14, mwaka huu.

Katika kesi hiyo, Kafulila ambaye alikuwa mgombea katika uchaguzi wa mwaka jana kupitia Chama cha NCCR- Mageuzi anaiomba mahakama imtangaze yeye mshindi kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi kifungu Na. 112 (c) kwa hoja kwamba alipata kura nyingi kwa mujibu wa matokeo ya kila kituo yaliyomo katika fomu Na. 21B  na kwamba msimamizi wa uchaguzi, alimtangaza Mwilima kinyume na matokeo halisi.

Kafulila anawakilishwa na jopo la mawakili wasomi, wakiongozwa na Tundu Lisu ambao ni Profesa Abdalah Safari na Daniel Lumenyera, huku Mwilima akiwakilishwa na Wakili Kennedy Fungamtama akiongoza jopo la mawakili wa Serikali wanaomwakilisha pia Msimamizi wa Uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama washtakiwa katika kesi hiyo.

Akizungumza nje ya mahakama, Kafulila alisema anakubaliana na uamuzi wa mahakama wa kuhairisha kesi hiyo. Hata hivyo aliwataka wapiga kura wake wawe na subira wakati wanasubiri tarehe ya kesi iliyopangwa ifike.

Post a Comment

 
Top