0


Kocha mkuu wa Mwadui FC Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ameiambia timu ya Simba kwamba inalaana ndiyo sababu ya kushindwa kufanya vizuri kwenye michuano ya ligi kuu Tanzania bara kwa muda mrefu.

Julio anadai laana hiyo inatokana na uongozi wa Simba kumfukuza yeye pamoja na kocha mkongwe Abdallah Kibadeni ‘Kin Kibadeni Mputa’ bila kuwalipa stahiki zao.

“Wakati mimi na King Kibaden tunafukuzwa Simba, niliwaambia kwamba ,mnatufukuza huku tunadai mishahara yetu na hiyo itakuwa laana kwasababu sisi tunafamilia kubwa ambazo zinatutegemea lakini wao walitufukuza hihuni”, anasema Julio ambaye ameshawahi kuitumikia Simba kama mchezaji na baadaye kama kocha.

“Niliweka nadhili kwenye ligi hii baada ya kuipandisha Mwadui lazima niifunge Simba, mechi ya kwanza tulitoka sare, walichomoa goli. Haji Manara akasema kuna goli walitufunga likakataliwa, safari hii tumekuja kwenye uwanja wao waliouzoea na tumewafunga.”

“Tukubali kwamba timu ya Simba mbovu na mimi nitoe wito kwa viongozi wa Simba, kama wanataka timu ifanikiwe lazima wawe wanatoa nafasi kwa waalimu wasajili wachezaji. Haya mambo ya mtu mwenye nguvu ya pesa ndiyo asajili wachezaji ni makosa kwasababu kitaalamu hata Mungu kazi nyingine hazitaki ndiyo maana kazi ya kuua kampa Israel.”

“Nimefurahi sana kuifunga Simba kwasababu wanapokuwa hawana kocha wananiita, wakipata kocha mzungu wa kumlipa pesa nyingi wananitimua tena kwa matusi.”

Maneno hayo ya Julio yamekuja mara baada ya Mwadui kuichapa Simba kwa bao 1-0 kwenye mchezo wa VPL uliochezwa Jumapili kwenye uwanja wa taifa.

Post a Comment

 
Top