Kiongozi wa
upinzani wa Kenya, Bw Raila Odinga ameikosoa Mahakama ya Kimataifa ya
Uhalifu wa Kivita (ICC) kwa kusitisha kesi ya uhalifu dhidi ya binadamu
iliyokuwa ikiwakumba vigogo wa serikali ya taifa hilo.
Rais Uhuru Kenyatta aliondolewa mashtaka dhidi yake Desemba mwaka 2014.
Zaidi ya watu 1,000 waliuaua na maelfu wengine kuachwa bila makao vurugu zilipozuka nchini Kenya kufuatia mzozo kuhusu matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2007.
Kiongozi huyo, ambaye alihudumu kama Waziri Mkuu baada ya ghasia hizo, anasema hatua hiyo ya ICC kuondoa mashtaka dhidi ya Wakenya itajenga kasumba ya kiburi miongoni mwa viongozi wa Afrika.
Akizungumza katika mji mkuu wa Ufaransa Paris, waziri mkuu huyo wa zamani alisema hatua ya mahakama ya ICC ya kufutilia mbali kesi za washukiwa wakuu katika ghasia mbaya zaidi kuwahi kutokea nchini Kenya tangu taifa hilo lijinyakulie uhuru, itawafanya viongozi wengi barani Afrika kutozingatia mfumo wa sheria wanapotawala. Bw Odinga alidai kwenye mahojiano na shirika la habari la AFP kwamba kutokana na uamuzi huo wa ICC, viongozi wengi wa kiafrika watakuwa madikteta na hawataogopa kushtakiwa na ICC kwa vile wanaweza kuhitilafiana na ushahidi bila kujali madhara yake.
Amesema mahakama ya ICC ilihadaiwa na Umoja wa Afrika kufutilia mbali mashtaka ya uhalifu dhidi ya binadamu ambayo yalikuwa yanawakabili washukiwa hao wakuu.
Matamshi hayo ya Bw Odinga hata hivyo yamepingwa vikali na baadhi ya wanasiasa nchini Kenya.
Bw Kamau Ichungwa, ambaye ni mbunge kutoka chama tawala cha Jubilee, amesema kiongozi huyo ameonesha unafiki.
“Yeye anajua chanzo cha vurugu zilizotokea Kenya. Na yeye ndiye mnufaika mkuu. Wakati Wakenya walipokuwa wakitoa vurugu walikuwa wakisema iwapo Raila hayuko hakuna amani. Alipoingia serikalini na akawa waziri mkuu, vurugu ziliisha,” ameambia BBC.
Badala yake amesema jambo litakalosababisha kuwepo kwa desturi ya kutoheshimu sheria "basi ni viongozi wa kisiasa kutumia vita na vurugu kujifaidi na kujitafutia vyeo.”
Post a Comment