Adolph Rishard awapa Yanga mbinu
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Kagera Sugar, Mohammed Rishard `Adolph’ aliyewahi kuichezea Yanga, ameionya klabu yake hiyo ya zamani akisema inapaswa kuwa makini na staili yao ya kucheza pasi nyingi na fupi.
Adolph aliyechezea pia klabu za Pan African, Pamba na pia kucheza soka ya kulipwa Austria na Oman, amesisitiza kama kweli inataka kupata matokeo mazuri dhidi ya Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kuanzia mwishoni mwa wiki hii, Yanga watapaswa kubadilisha mfumo.
Yanga itakuwa mwenyeji wa Al Ahly Jumamosi wiki hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na timu hizo zitarudiana wiki moja baadaye huko Misri.
Akizungumza juzi mara baada ya Kagera Sugar kulambwa 3-1 na Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara jijini Dar es Salaam, Adolph, kiungo mahiri wa zamani wa kimataifa nchini, alisema Yanga wamekuwa wakicheza sana mchezo wa pasi nyingi ambao unapoteza muda na pia hukaribisha wapinzani kushambulia.
“Nilivyowatazama Yanga wanacheza mchezo wa pasi nyingi kuliko kufunga, na hata wakipata nafasi zenyewe wanashindwa kuzitumia, wanahitaji kubadilika la sivyo wako hatarini kupoteza,” alisema.
Wakati Adolph akiiona dosari hiyo, Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm amekiri bado timu yake imekuwa na tatizo sugu la kupoteza nafasi.
Pluijm hakufurahishwa na matokeo ya 3-1 dhidi ya Kagera Sugar, akisema ni machache tofauti na wanavyoonekana kuyapokea vyema mafunzo wanapokuwa mazoezini.
Hata hivyo, ameahidi kuzifanyia kazi dosari mbalimbali wakati wa kambi yake ya siku tano kuanzia jana huko visiwani Pemba ilikokwenda kuweka kambi mahsusi kwa mchezo dhidi ya Al Ahly.
Post a Comment