0


ADHABU za Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Nchini (TFF) dhidi ya wadau wa michezo wanaohusishwa na upangaji wa matokeo katika Kundi C la Ligi Daraja Kwanza msimu huu, limemgusa aliyekuwa Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia na kuitaka serikali kuingilia kati.

Juzi, kamati hiyo chini ya Makamu Mwenyekiti wake, Jerome Msemwa iliwafungia kujihusisha na soka maisha viongozi saba wa soka kwa kukutwa na kosa hilo katika mechi za kundi C.
Akizungumza na kituo kimoja cha redio nchini jana, Nkamia ambaye ni mbunge wa Kondoa Kusini alisema adhabu iliyotolewa kwa wahusika ni kubwa na kwamba ipo haja kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kuingilia kati suala hilo.

Mbali na kufungiwa kwa viongozi hao kamati hiyo pia imefungia wachezaji wawili na waamuzi wawili kujihusisha na soka kwa miaka 10 kila mmoja huku wakipigwa faini ya Sh milioni 10 kila mmoja.
Aidha kamati hiyo imezishusha mpaka daraja la pili timu za Geita Gold (Geita) iliyokuwa ipande Ligi Kuu, JKT Oljoro (Arusha) na Polisi Tabora (Tabora) huku JKT Kanembwa ya Kigoma

ikishushwa mpaka hatua ya ligi ya mkoa (RCL) baada ya kukutwa na hatia za kupanga matokeo.
Alisema; “Kilichonishtua mimi kama mwandishi wa habari za michezo wa siku nyingi, kiongozi wa klabu (Simba) na pia nimewahi kuwa Naibu Waziri wa michezo lakini pia kama mwanamichezo ni adhabu kubwa sana zilizotolewa kwa watu… Kumpa mtu adhabu ya maisha au miaka 10 au mchezaji wa ligi daraja la kwanza kumwambia alipe faini ya Sh milioni 10 anaipata wapi? “Nadhani upo

umuhimu wa ile kamati kukaa chini na kupitia maamuzi yake, ni kweli kupanga matokeo ni tukio lenye adhabu kubwa sana, lakini kumpa mtu adhabu ya maisha au miaka 10 au mchezaji wa ligi daraja la kwanza alipe Sh milioni 10 sidhani kama wana uwezo huo… halafu asipolipa hizo fedha inakuwaje…,” alisema.

Aliendelea: “Mimi kama Nkamia nadhani adhabu kama miaka mitatu kulipa faini ya laki tano wanaweza kulipa, lakini leo mchezaji ambaye mpira ndiyo maisha yake na inawezekana ameshinikizwa na watu wengine kufanya haya unampa adhabu ya miaka 10 na kulipa shilingi milioni 10 au unamfungia maisha nadhani sio uungwana.”

Waliofungiwa maisha ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoa wa Tabora, Yusuph Kitumbo na Katibu wake, Fateh Rhemtullah, Mwenyekiti wa JKT Oljoro, Amos Mwita na Kocha Msaidizi wa Polisi Tabora, Bernard Fabian.

Wengine waliofungiwa maisha ni mwamuzi wa mchezo kati ya JKT Kanembwa FC v Geita Gold, Saleh Mang’ola, Kamisaa wa mchezo huo, Moshi Juma na Kocha Msaidizi wa Geita Gold, Choke Abeid.

Wachezaji waliofungiwa miaka 10 ni kipa Mohammed Mohammed wa JKT Kanembwa na Dennis Richard wa Geita Gold huku wakitakiwa pia kulipwa faini ya sh milioni 10 kila mmoja.

Post a Comment

 
Top