0

anaongoza kwa wajumbe katika chama cha Republican
Mgombea urais wa chama cha Republican nchini Marekani Donald Trump amesema viongozi wa chama hicho hawataki ashinde uteuzi wa chama hicho.

Akizungumza mjini New York, mfanyabiashara huyo tajiri amesema Kamati ya Taifa ya Republican (RNC) inapanga njama dhidi yake.

Amesema hayo baada ya mpinzani wake Ted Cruz kupewa wajumbe wote katika jimbo la Colorado licha ya kuwa upigaji kura haukufanywa jimbo lote.

Bw Trump anaongoza kwa wajumbe katika kinyang’anyiro cha kuteua mgombea urais wa chama hicho lakini huenda akashindwa kupata wajumbe wa kumkabidhi ushindi wa moja kwa moja.

Hili huenda likapelekea kuwepo kwa mkutano wenye ubishi Julai, wakati wa kuidhinisha mgombea.
Katika mkutano kama huo, wajumbe watakuwa huru baada ya kura ya kwanza kupigwa kumuunga mkono mgombea yeyote.

Hili litafungua njia kwa Seneta wa Texas Bw Cruz au hata John Kasich kuidhinishwa.

Gazeti la Washington Post liliandika Jumatano kwamba Bw Cruz huenda akashinda kura ikipigwa mara ya pili kwa sababu amewashawishi wajumbe wengi kumpigia kura hali kama hiyo ikitokea.
Lakini mwenyekiti wa RNC Reince Priebus amekana madai ya Bw Trump kwamba sheria ilibadilishwa katika jimbo la Colorado kumnyima wajumbe.
 
Bw Priebus amekana madai ya Trump
Bw Priebus ameandika kwenye Twitter kwamba utaratibu wa uteuzi ulifahamika wazi kwa zaidi ya mwaka mmoja.

“Ni wajibu wa wanaofanya kampeni huufahamu. Unalalamika sasa? Pole.”


Alipoulizwa katika mkutano mmoja katika mji wa New Yrk iwapo kamati hiyo kuu inataka ashinde, Bw Trump alisema: “Hapana, sidhani. Sidhani kamwe.”

Bw Trump ameshutumiwa kwa kutofanya kampeni za kutosha katika majimbo kama vile Colorado.
Lakini Trump amesema wajumbe waliotaka kumuunga mkono walitimuliwa na RNC.

"Hawanitaki kwa sababu natumia pesa zangu. Kwa sababu hii ina maana kwamba hawawezi kunidhibiti kwa sababu nafanyia kazi raia,” amesema.

Post a Comment

 
Top