0

MANCHESTER, ENGLAND
FERGUSONKOCHA wa zamani wa klabu ya Manchester United, Sir Alex Ferguson, anaamini kuwa klabu ya Leicester City ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu nchini England msimu huu.

Kocha huyo amedai umoja wa wachezaji wa klabu hiyo wanamkumbusha wakati anaifundisha Manchester United huku ikitwaa ubingwa.

Leicester City kwa sasa inaongoza Ligi ikiwa na alama 66, ikiwaacha Tottenham alama tano ambao wanashika nafasi ya pili, lakini Ferguson amesema klabu hiyo itachukua ubingwa msimu huu kutokana na michezo iliyobaki.

“Huu ni wakati wao Leicester City, wana kila sababu ya kutwaa ubingwa msimu huu, wanachotakiwa kukiangalia kwa sasa ni jinsi gani ya kumaliza michezo iliyobaki bila kupoteza kwa kuwa Tottenham nao wapo katika kipindi kizuri.

“Ushindi wa bao 1-0 ni hatari, unatakiwa kushinda zaidi ya bao, Leicester michezo yao mitatu ya mwisho wameshinda ushindi huo wa bao moja, hata wakati naifundisha Man United msimu wa mwaka 1996-97 nilishinda michezo nane ya mwisho kwa ushindi wa bao 1-0 na kuchukua ubingwa,” alisema Ferguson.

Kocha huyo amewamwagia sifa washambuliaji wa Leicester, Jamie Vardy na Riyad Mahrez, kwamba wana mchango mkubwa katika klabu hiyo wa kuhakikisha inafanya vizuri msimu huu.

Post a Comment

 
Top