0



Pg 32TIMU ya Yanga na Azam FC zimefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), baada ya kuibuka na ushindi katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

Yanga ambayo ilikuwa ikicheza katika Uwanja wa Taifa wa jijini Dar es Salaam, ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ndanda FC huku Azam iliyokuwa ikicheza Uwanja wa Azam

Complex ilifanikiwa kupata ushindi mnene wa mabao 3-1 dhidi ya timu ya Tanzania Prisons ya Mbeya.
Mabao ya Yanga yalifungwa na mshambuliaji wake mahiri Paul Nonga dakika ya 26 na Kelvin Yondani dakika ya 69, ambapo Azam ilipata mabao yake kupitia kwa Shomari Kapombe dakika ya (9,52) na Khamis Mcha dakika ya 86.

Mpira ulianza kwa Ndanda kupata bao dakika ya sita kupitia mshambuliaji wake, Atupele Green lakini lilikataliwa baada ya mshika kibendera kuonesha kuwa alikuwa ameotea.

Bao hilo liliwapa nguvu Ndanda ya kushambuliana mara kwa mara, lakini Yanga ilifanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya 26 kupitia kwa Paul Nonga akimalizia vema mpira wa faulo uliopigwa na Juma Abdul.

Yanga ilijikuta ikikosa bao la pili dakika ya 34 baada ya shuti lililopigwa na Simon Msuva nje ya 18 kugonga mwamba na kutoka nje.

Hadi mwamuzi Jimmy Fabuel kutoka Shinyanga anapuliza kipyenga kuashiria mapumziko, Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0 licha ya timu zote kushambuliana kwa zamu tangu mwanzo wa mchezo.

Ndanda ilianza kipindi cha pili kwa kasi na kuandika bao la kusawazisha dakika ya 56 kupitia kwa mshambuliaji wake Kigi Makasy aliyepiga shuti kali nje ya 18 lilomshinda kipa wa Yanga, Deogratius Munisi na kutinga wavuni.

Watoto hao wa Jangwani walipata bao la pili kwa mkwaju wa penalti lililofungwa na Kelvin Yondani dakika ya 69, baada ya Msuva kuchezewa vibaya na beki wa Ndanda, Paul Ngalema  akiwa ndani ya 18 ambaye alitolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kitendo hicho.

Bao hilo liliizindua Ndanda na kutaka kusawazisha dakika ya 90 kupitia Brayson Raphael, baada ya kuachia shuti lililotoka nje kidogo ya goli.

Katika mchezo ulioikutanisha Azam na Prisons, mchezo huo ulianza kwa kasi ya kila timu ikionekana kutaka bao la mapema.

Azam ilifanikiwa kupata bao dakika ya tisa kupitia kwa  Shomari Kapombe, aliyepokea pasi nzuri kutoka kwa Didier Kavumbagu.

Prisons walisawazisha bao hilo katika dakika ya 30, mfungaji akiwa Jeremiah Juma baada ya kutumia uzembe wa mabeki wa Azam kwa kupiga shuti ndani ya 18, ambalo lilimshinda kipa wa timu ya Azam, Aishi Manula na kutinga wavuni.

Bao hilo liliwafanya Prisons kuzinduka ambapo dakika ya 40, Jeremiah alikosa bao baada ya Manula kupangua shuti lililopigwa na mshambuliaji huyo.

Baada ya kucheza mpira wa kasi kwa kila timu kutaka nafasi ya kuongeza bao la pili, timu hizo zilijikuta zikienda  mapunziko zikiwa sare ya bao 1-1.

Azam iliingia kipindi cha pili na kuandika bao la pili dakika ya 52 kupitia kwa Kapombe, akiunganisha pasi safi ya Abubakar Salum ‘Sure Boy’ na kutumia juhudi binafsi akiwa nje ya 18 na kupiga shuti lililokwenda  moja kwa moja  wavuni.

Timu hiyo iliendelea kulishambulia lango la Prisons na kufanikiwa kuongeza bao la tatu dakika ya 86, mfungaji akiwa Khamis Mcha baada ya kufanikiwa kuwapita mabeki wa Prisons na kufunga.

Post a Comment

 
Top