0

CHANGAMOTO ya uhaba wa madawati katika shule nyingi za msingi nchini imeongezeka mara dufu mwaka huu kutokana na serikali kuanza utekelezaji wa mpango wa elimu bila malipo.
Shule nyingi zimejikuta zikiandikisha wanafunzi wengi waliojiunga na madarasa ya awali pamoja na darasa la kwanza.

Wanafunzi wakiwa darasani.Ukubwa wa changamoto hii umezilazimu halmashauri mbalimbali nchini kuibuka na mikakati ya kuweza kukabiliana nalo, miongoni mwa halmashauri hizo ikiwa ya Mbarali mkoani Mbeya.

Hii ni moja ya halmashauri sita zinazounda Mkoa wa Mbeya, ina shule za msingi 112, kati ya hizo 109 ni za serikali zenye wanafunzi 49,724, wavulana 24,079 na wasichana 25,645.

Mwanzoni mwa mwaka huu wilaya hiyo ilisajili wanafunzi 19,046 kwa madarasa ya awali na la kwanza, idadi ambayo ilikuwa takriban mara mbili ya kiwango kilichokuwa kikitarajiwa awali.
Fanikio hili likaja na changamoto ya ongezeko la uhaba wa madawati, ambalo tangu awali lilikuwa likiikabili halmashauri hii.

Tathmini iliyofanywa na wataalamu wa halmashauri ikabainisha kuwa shule za wilayani humo zina madawati 12,889 tu huku mahitaji yakiwa ni madawati 18,860.

Hii ikimaanisha kuna upungufu wa madawati 5,971.

Aidha, wataalamu hao wakapiga hesabu za wastani wa kila dawati kwa bei za kawaida za mitaani na kubaini kuwa halmashauri ingeweza kutumia zaidi ya Sh milioni 800 kuweza kuondosha tatizo hilo, kwa wastani wa kila dawati ni Sh 140,000.
Kiasi hiki ni kingi kwa halmashauri hii ambayo kwa kiasi kikubwa inategemea kilimo, huku miundombinu ya umwagiliaji ikiwa haijatosheleza, hivyo inakabiliwa na changamoto nyingi zaidi ya hiyo ya madawati.

Ndipo likaja wazo la halmashauri kuwa na karakana yake ili kutengeneza madawati hayo hali ambayo si tu kuwa itapunguza gharama za kutengeneza madawati hayo bali pia kutengeneza nafasi za ajira kwa vijana wenye ujuzi wa useremala wilayani hapo.

Mkakati huo utaiwezesha halmashauri hiyo kupunguza matumizi ya fedha za madawati hadi kufikia Sh milioni 235 kutoka milioni 800 ambazo ingetumia kama ingechukua wazabuni.

Upungufu huo wa gharama umetokana pia na ushirikishwaji wa wananchi katika kata zote 20 zinazounda wilaya hiyo, ambapo kila kata itachangia magogo yatakayochanwa na kupatikana mbao kwa ajili ya kufanikisha utengenezaji huo wa madawati.

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Yeremiah Mahinya, anasema wana uhakika wa zoezi hilo kufanikiwa haraka iwezekanavyo, hasa kwa kuwa kumekuwa na mwitikio mkubwa wa wananchi katika kushirikiana nao ili kuondokana na tatizo la watoto kusoma wakiwa wamekaa chini.

“Ukiachilia mbali vijiji viwili tu ambavyo hadi sasa vimesuasua kuchangia magogo kwa ajili ya kuchana mbao, vijiji vingine vilivyosalia vilishatoa magogo ili kutatua tatizo la watoto kusoma katika mazingira magumu,” anasema mkurugenzi huyo.

Utekelezaji wa mkakati huu ambao uko katika awamu mbili, umeshashuhudia awamu ya kwanza ambayo ilipangwa kukamilika mwishoni mwa Februari mwaka huu, ikikamilika kwa utengenezaji wa madawati 4,281 huku sehemu ya pili ikitarajiwa kukamilika kwa kumalizia madawati 1,690 yaliyosalia.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, utekelezaji wa mpango huo ambao ulianza tangu mwaka 2014, ulianza kwa harambee ya uchangiaji madawati iliyokuwa imeitishwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Hussein Kiffu, ambapoSh 112,261,000zilipatikana.
Aidha, wananchi walishirikishwa ambapo waliombwa kuchangia Sh milioni 104, ingawa kiasi kilichokusanywa kilikuwa milioni 98 tu.
Wadau wengine kadhaa pia walijitokeza kusaidia kufanikishwa kwa mkakati huu ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, ambao walichangia Sh milioni 7.
“Kwa ujumla tuliweza kukusanya Sh milioni 218 na hadi sasa tumeshatumia Sh milioni 216, ili kufanikisha awamu hii ya kwanza ya utengenezaji wa madawati,” anasema.
Hatua hii ya halmashauri ya Mbarali, ilimvutia naibu Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jaffo, ambaye hivi karibuni alitembelea halmashauri hiyo kukagua shughuli za maendeleo pamoja na kukutana na watendaji wa halmashauri hiyo.
Mara baada ya kupokea taarifa ya utekekezwaji wa mpango huo, Jafo akazitaka pia halmashauri zingine nchini kuiga mfano huo wa kupunguza gharama za mahitaji mbalimbali ya kimsingi kama hilo la madawati kwa kuwa na karakana zao.
“Kwa kuangalia mchanganuo huu utaona ni kiasi gani halmashauri imeweza kuokoa kiasi kikubwa cha fedha ambazo zitatumika kwenye shughuli zingine za kuwaletea maendeleo wananchi na hili linawezekana kufanyika kwenye halmashauri zingine pia,” anasema Jafo.
Anasema ni lazima watendaji wawe wabunifu kwa sababu mahitaji ya wananchi ni mengi na yote ni ya msingi.
“Fedha zilizopo haziwezi kutosheleza kila kitu, kwahiyo kama kuna uwezekano wa kuwa na mikakati ya halmashauri kubeba baadhi ya kazi kwa kiwango hiki, mtakuwa mnaisaidia serikali kufikia malengo ya kuwaletea wananchi maisha bora kwa haraka zaidi,” anasema.
Aidha Naibu waziri huyo akatumia fursa hiyo kuagiza vijiji kadhaa ambavyo vilikuwa havijachangia magogo, kutekeleza agizo hilo haraka iwezekanavyo, la sivyo wachukuliwe hatua za kisheria kwani watakuwa wanahujumu harakati za kuwapatia wanafunzi mazingira mazuri ya kujifunzia.
“Misitu ni ya serikali, watoto wanaosoma ni wao na ni wetu sote, haiwezekani baadhi waone kuna umuhimu na kujitolea rasilimali walizonazo, kisha wengine wakaidi kufanya hivyo, hii ni kukwamisha harakati za halmashauri na za wananchi wenzao katika kuweka mazingira bora kwa wanafunzi kupata elimu,” anasema Jafo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amosi Makala, anasema kila halmashauri inatakiwa kuwa na takwimu sahihi juu ya uhaba wa madawati.
“Pamoja na juhudi kubwa ambazo zimefanywa na halmashauri mbalimbali zamkoa huu upande wa elimu, naomba wakurugenzi katika halmashauri husika wahakikishe wana takwimu sahihi hasa za uhaba wa madawati ili kuwezesha mkoa kuwa na mikakati ya uhakika ya kulishughulikia,” anaagiza mkuu huyo wa mkoa.

Post a Comment

 
Top