0
DSC_0889

UJENZI wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Bandari ya Tanga, haujaharibu urafiki na uhusiano wa  biashara kati ya Tanzania na Kenya.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Balozi wa Tanzania nchini Kenya, John Haule, alipozungumza na MTANZANIA kuhusu   ujenzi wa bomba hilo ambalo awali Serikali ya Uganda ilipanga kuitumia Bandari ya Lamu ya Kenya.

Balozi alisema   ujenzi wa bomba hilo hadi bandari Tanga siyo gumzo  Kenya na hakuna anayefuatilia wala kujali kuhusu suala hilo, si wananchi wa Kenya wala viongozi wao.

“Huku tuko vizuri kabisa, suala hilo wala halizungumzwi na hata vyombo vya habari havijalipa kipaumbele kama ilivyo Tanzania, si tatizo kwa hapa,” alisema Haule.
 `
Alisema  suala hilo lisingeweza kuharibu uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Haule alisema ubalozi umekuwa ukipewa barua kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya ikielekeza jinsi unavyotakiwa kuendesha shughuli zake na kuwasaliana na mamlaka za Kenya.
Alisema pamoja na mambo mengine, maofisa wa ubalozi  hawaruhusiwi kupokea viongozi wala kwenda kwenye mikutano nchini Kenya bila  ruhusa wizara.

Balozi huyo alisema kwa sababuhiyo alishangazwa na kitendo cha maofisa waandamizi wa Kenya akiwamo Waziri wa Nishati, Charles Keter, kutaka kwenda Tanga bila ya kuwasiliana na ubalozi wa Tanzania nchini humo.

“Waligundua wamefanya makosa ndiyo maana baada ya tukio hilo kumekuwa kimya kabisa. Uganda walibaini unafuu mkubwa wa kupitisha bomba Tanzania hivyo sidhani kama kuna tatizo,” alisema.
Pamoja na mambo mengine, Haule alisema kuwa kuanzishwa kwa safari za Fastjet hadi Nairobi kumesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha uhusiano wa  biashara kati ya nchi hizo mbili.

Alisema miongoni mwa wawekezaji katika Tanzania, Wakenya wanaongoza hivyo anapata matumaini makubwa   kwamba uhusiano huo utazidi kuboreshwa kupitia shirika hilo la ndege.
“Tuna tatizo la kutokuwa na kampuni ya ndege ya kimataifa  na ndege zilizopo hazitoshi kutokana na idadi ya wafanyabiashara waliopo.

“Naamini Fastjet itasaidia kuziba pengo lililokuwapo awali hasa ukizingatia jinsi wanavyotekeleza majukumu yao kwa kutoa huduma bora,” alisema.

Alisema  shirika hilo lina nafasi kubwa ya kudumisha uhusiano huo na ni mwanzo mzuri.
Haule alisisitiza kuwa ubalozi wa Tanzania nchini Kenya unaitegemea Fastjet katika kutekeleza masuala yake  ya  uchumi kwa kuwa inachangia kuongeza watalii ambao wamehamasika kupanda ndege  kutalii Tanzania ikizingatiwa haitozi gharama kubwa za usafiri.

Post a Comment

 
Top