0

IGP_ErnestMangu4
*Ni ule uliohusisha vigogo wa Serikali, Jeshi la Polisi
*Watumia bilioni 5/- mafunzo kwa watu watano

MKATABA tata wa Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd inayomilikiwa na mfanyabiashara Said Lugumi, umezidi kuchukua sura mpya baada ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kushindwa kuendelea na sakata hilo kutokana na kuhamishiwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Hatua hiyo inatokana na utata uliogubika mkataba huo ambao unawahusisha vigogo kadhaa wa Jeshi la Polisi pamoja na baadhi ya watendaji wa Serikali ya Rais Dk. John Magufuli, huku ikidaiwa kuwa huenda ikawa njia ya ‘kulindwa’.

Wiki iliyopita PAC ilipokutana na jeshi hilo kupitia taarifa ya hesabu zao za mwaka 2013/14
zilizokaguliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ilibainika kuwa mwaka 2011 liliingia mkataba na kampuni hiyo kwa ajili ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo vya polisi 108 nchi nzima kwa gharama ya Sh bilioni 37.

Lakini hadi sasa mashine hizo zimefungwa katika vituo 14 pekee na kampuni hiyo kulipwa Sh bilioni 34 ambazo ni sawa na asilimia 99 ya fedha za makubaliano ya mkataba.

Kutokana na hali hiyo, PAC ambayo ilibaini kuwapo viashiria vya ufisadi katika tenda hiyo, iliwaagiza watendaji wa jeshi hilo kuwasilisha taarifa za mkataba huo pamoja na vielelezo vyake ili wajumbe waweze kuupitia pamoja na kutoa maagizo.

Chanzo cha kuaminika kiliambia MTANZANIA kuwa katika sehemu ya mkataba huo kati ya Jeshi la Polisi na Lugumi, imebainika kampuni hiyo kufanya mafunzo kwa watu watano ambayo wametumia Sh bilioni 5, huku mshauri mwekelezi akilipwa Sh bilioni 46 nje ya fedha zilizopo kwenye mkataba.
Hatua ya mkataba huo kupelekwa mbele ya Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, inadaiwa kuwa njia ya kutaka kuwalinda baadhi ya vigogo ambao wanatajwa kuhusika na kashfa hiyo ambayo imelitia doa Jeshi la Polisi nchini.

“Hapa kuna kulindana tu, hakuna namna yoyote. Kama uchafu umebainika mbele ya Kamati ya PAC inakuwaje wengine wanadaka kitu ambacho hakikuanza kwao?

“Kuna kila dalili ya wingu na shaka, ila ukweli utajulikana tu, haiwezekani watu wanatumia fedha za walipakodi vibaya halafu inapokuja wanataka kushughulikiwa wanatafuta kivuli cha kujifichia,” kilisema chanzo chetu.

Mkataba huo uliibuliwa na PAC wiki iliyopita ambapo watendaji wa Jeshi la Polisi walishindwa kutoa maelezo ya kutosha ndipo ikawataka kuwasilisha taarifa juzi.

Pamoja na kutakiwa kufanya hivyo, hadi kufikia jana saa 10 jioni Makamu Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hilaly, alisema kuwa kamati yao haijapokea taarifa yoyote kuhusu Kampuni ya Lugumi hivyo wameliandika barua Jeshi la Polisi liwasilishe mkataba huo ndani ya siku tatu.

Alisema barua hiyo wamemuomba Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah,  ili aweze

kuwaandikia Polisi ili wawasilishe mkataba huo kwa mujibu wa utaratibu kama kamati ilivyoagiza.
“Hadi muda huu ninapozungumza nawe sijapata taarifa yoyote, kwa hali hiyo tumelazimika

kumwandikia barua Katibu wa Bunge ili awaandikie barua polisi walete mkabata huo ndani ya siku tatu kutoka leo (jana) kama walivyotakiwa na kamati yetu,” alisema Hilaly.

BALOZI ADADI
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Balozi Adadi Rajabu, alithibitisha mkataba huo kuwasilishwa mbele ya kamati yake.

“Mimi kama mwenyekiti wa kamati ninapenda kukiri kwamba tumepokea mkataba kati ya Jeshi la Polisi na Kampuni ya Lugumi na tutaufanyia kazi kwa kina.

“Tunahitaji kuona kama kuna wizara zilizohusika na mkataba huu na kama tutaukuta ni mbaya, tutatoa taarifa kwa umma. Kikubwa tunawaomba Watanzania wawe watulivu, hatuko kwa ajili ya kumlinda mtu wala kikundi cha watu, tunasimamia masilahi ya Watanzania wote,” alisema Balozi Adadi.

RIDHIWANI AKANA

Taarifa za mkataba huo zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii zikiwahusisha baadhi ya vigogo wa Serikali akiwamo Waziri wa Serikali ya Rais Magufuli pamoja na kumtaja Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete (CCM).

Hata hivyo, Ridhiwani alivunja ukimya na kukanusha taarifa hizo zilizodai yeye ni mmoja wa wamiliki wa Kampuni ya Lugumi pamoja na Said Lugumi na aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Said Mwema.

Akizungumza na gazeti moja la kila siku (Si MTANZANIA), Ridhiwani ambaye ni mtoto wa Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, alisema hahusiki na Lugumi ingawa wana urafiki wa kawaida na mmiliki wa kampuni hiyo.

“Kwanza kabisa mimi si mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo, hilo ni jambo la msingi kabisa watu waelewe, na sijawahi kufanya biashara yoyote na Lugumi. Said Lugumi ambaye ni mmiliki wa kampuni hiyo tunafahamiana naye na ni rafiki yangu,” alisema Ridhiwani.

Alisisitiza kuwa hana uhusiano wa kibiashara na mtu huyo na kwamba hafahamu ni kwanini amehusishwa na Kampuni ya Lugumi.

“Hapa ni watu tu wanaamua kuingiza tu maneno yao, haya maghorofa ninayotajwa kumiliki Dar es Salaam hata sijawahi kutembelea ujenzi wake, wameamua kuniingiza, Lugumi nafahamiana naye binafsi tu lakini wananiingiza,” alisema Ridhiwani.

Post a Comment

 
Top