JUMAMOSI
iliyopita niliandika na kuelezea namna safari yangu ya kwenda Hispania
ilivyokuwa na namna nilivyowaza kama ningepata nafasi ya kuhojiana na
wachezaji nyota kabisa duniani kama Lionel Messi, Luis Suarez na Neymar.
Wako
wengi nilitamani kuwapata kama Dani Alves, Iniesta, Sergio Bosquet na
wengine ambao kila mwandishi au kila chombo cha habari kingependa
kuzungumza nao mawili matatu na kuandika au kuripoti.
Nilieleza
namna hata wenyeji wetu ambao ni La Liga ambao ndiyo wanaongoza Ligi
Kuu ya Hispania, walionekana kuzungumzia ugumu wa kuwapata watu hao
wenye ulinzi mkubwa kupita unavyojua.
Nimeripoti
kwenye Michuano ya Kombe la Dunia, Kombe la Mataifa Afrika na mechi
kadhaa za kimataifa. Sijawahi kuona ulinzi mkali kama wa wachezaji hao.
Mfano
nilielezea namna wachezaji kama Messi, Neymar, Iniesta, Suarez
walivyoongozwa na mabaunsa hata walipopita kwenye Mixing Zone (hii ni
sehemu maalum ya waandishi wa habari kwa ajili ya kuwahoji wachezaji
wakati wakiondoka kwenda kwenye basi lao). Nilishangaa, yaani kwa Messi,
Suarez, Iniesta na Neymar hata waandishi hawaaminiwi!
Pamoja
na yote hayo, juhudi zilifanyika, waliulizwa maswali, baadhi walijibu
na wengine la. Hakika haikuwa rahisi kutokana na mazingira yake.
Kabla
ya hapo, nilifanikiwa kujifunza namna wachezaji wa timu za La Liga
wanavyoingia uwanjani, namna mashabiki wanavyoonyesha hamu kuu ya
kuwaona na ulinzi mkali unaowekwa kuhakikisha tuko salama.
Mimi
ninaposafiri, ninakwenda kwa niaba ya chombo cha habari
ninachokitumikia. Kama ni rekodi mpya, Gazeti la Championi ndiyo
limefika katika hatua nyingine mpya ambayo itakuwa mfano na changamoto
kwa wengine.
Kama
unakumbuka, miaka zaidi ya mitano iliyopita, nilifunga safari hadi
Malawi kumfuata Didier Drogba aliyekuwa nchini humo ambapo nilifanya
naye mahojiano ya ana kwa ana kabla ya kurudia tena jijini Dar es
Salaam.
Mahojiano
na Drogba, yaligeuka kuwa chachu ya waandishi wengi kuamini
inawezekana, wakatamani kusafiri na kufanya mahojiano sehemu mbalimbali.
Ilikuwa ni rekodi mpya na mapinduzi mapya yaliyofanywa na Championi na
kubadilisha aina uandishi, kuachana ule wa kusubiri kila kitu na sasa
kuanza kusaka mambo mapya ikiwezekana kwa safari ndefu na ngumu ili
kutimiza ndoto.
Safari
hii, Championi limefika mbali, karibu na Messi, lakini mambo hayakuwa
mazuri. Karibu na Suarez na mahojiano mafupi kwa kuwa alijibu swali kama
Alves, Neymar akaeleza hisia zake kwamba Kingereza hakipandi.
Inabaki
palepale, bado wasomaji wetu wanahitaji zaidi ya pale. Ugumu wake
hakika uko juu, lakini bado tunahitaji kupambana kwa ajili yao.
Najua
hili nalo litakuwa changamoto kwa wengine na sasa wanaweza kutamani
kufika mbali zaidi ikiwezekana England, Ujerumani na kuwapata wachezaji
wa Manchester United, Arsenal na wengine au wale wa Bayern Munich,
Dortmund na wengine.
Hakuna
anayeweza kukataa tena kwamba Championi limeandika rekodi nyingine mpya
ya ubunifu, uanzilishi na hii ni kwa niaba ya wasomaji.
Wasomaji
wa Championi lazima wajue, huenda tunalala kwa shida lakini tukiwaza
nini cha kuwapa sahihi. Safari yangu kwenda Hispania ilikuwa ndefu,
yenye maumivu ya uchovu na ratiba ndefu iliyopandana, lakini kila
nilipowafikiria wasomaji, nilisema; “Sitaki kuwaangusha”.
Huenda
sijafanikiwa kwa kiasi kitakachowaridhisha wote kwa asilimia mia
japokuwa bado tunaendelea kubuni, kuwazua na kujipanga kuweka rekodi
kibao na kuwapa wasomaji heshima yao ya kupata wanachotaka.
Niwashukuru
Azam TV kwa ushirikiano wao wa juu katika safari yangu ya Hispania. La
Liga pia ambao waliniamini na kunipa nafasi ya kufanya mengi ikiwa ni
pamoja na kwenye runinga na mtandao wao.
Kwa wasomaji, ninawaomba waendelee kutuamini na tunaendelea kupambana kwa ajili yenu.
Kwa
waandishi wengine, hii ni changamoto mpya kwenu, ushindani wetu
utaongeza ubora. Kwa wale mliokubali tunachofanya nanyi mkafanya vyenu,
ni vizuri sana. Wengine pia mnaweza kufuata ili tuifanye tasnia hii
yenye ushindani na mambo mapya na mazuri zaidi kwa wasomaji.
Kwa upande wetu Championi, sasa ndiyo asubuhi na mapema, wasomaji wetu shukurani kwenu.
Saleh Ally
Mhariri Kiongozi-Championi
Post a Comment