0


HALL (KUSHOTO) AKIWA NA KOCHA MKUU WA YANGA, HANS VAN DER PLUIJM

Kocha Stewart Hall wa Azam FC ‘amenunua’ ugomvi wa Yanga na Coastal Union kwa kusema kuwa kuna kila sababu ya kujifikiria mara mbili kwa nini kila siku itajwe Yanga katika matokeo tatanishi na kuongeza kuwa Yanga haikupata ushindi halali kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho.

Mchezo wa Yanga na Coastal ulivunjika katika dakika 15 za mwisho za nyongeza ambapo Yanga ilikuwa ikiongoza mabao 2-1, baada ya kupitia ripoti ya mchezo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likaipa Yanga ushindi kwa madai kuwa mashabiki wa Coastal walikuwa chanzo cha mchezo huo kuvunjika.

“Kila mtu, kila kona hapa gumzo ni mchezo huo wa Coastal na Yanga, hata katika mitandao ya kijamii na Youtube yanayozungumzwa sana kuhusu soka la Tanzania ni hujuma, limejaa viashiria vya rushwa,” alisema Hall na kuongeza:

“Niliona mchezo ule, bila kificho mabao yote hayakuwa halali, bao la kwanza aliotea (Donald Ngoma), bao la pili wazi kabisa lilikuwa la mkono, lakini mwamuzi hakuwa na maamuzi. TFF wanatakiwa kufunguliwa mashtaka.

“Nimekuwa hapa mwaka wa sita sasa, soka linatawaliwa na rushwa lakini kwa sasa imezidi kiwango.”

Tayari Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) ipo kwenye uchunguzi wa kina kwenye soka kubaini mianya ya rushwa ambacho kimekuwa kilio cha Watanzania kila kukicha. 


SOURCE: CHAMPIONI

Post a Comment

 
Top