Kundi la wadukuzi
wa mitandaoni la Anonymous limeshambulia tovuti ya wizara ya mambo ya
nje ya Kenya na kuiba data muhimu, tovuti moja ya usalama mtandaoni
imeripoti.
Operesheni hiyo ilizinduliwa mwaka jana.
Serikali ya Kenya haijasema iwapo kuna nyaraka na habari muhimu ambazo zimeibiwa na wadukuzi hao.
Tovuti ya HackRead inasema data ya jumla ya 1TB ambayo imeibiwa imeanikwa kwenye “mitandao ya giza” ambayo ni mitandao ambayo ina siri kuu na huficha majina na utambulisho wa wanaoitumia.
Anonymous majuzi walidukua tovuti ya kampuni ya kusafisha mafuta ya Kenya pamoja na tovuti za mashirika mengine yanayomilikiwa na serikali.
Udukuzi wa tovuti nyingi katika nchi za Afrika kusini mwa jangwa la Sahara hata hivyo sana huhusisha kuzichafua badala ya kuiba data.
Huku watu na serikali nyingi zikianza kufanya shughuli zaidi mtandaoni, kuna habari na maelezo mengi zaidi ambayo yanaweza kuandamwa na wadukuzi.
Anonymous hufanya kazi kama mtandao wa ushirika. Hushirikisha wadukuzi kutoka nchi mbalimbali ambao hutumia jina hilo na hivyo huwa vigumu kufahamu iwapo wadukuzi wanatoka nje ya nchi au ndani ya nchi.
Kundi hilo hujidai kuwa la wanaharakati ambao hutekeleza uvamizi wa mitandaoni kukabiliana na ufisadi na ukiukaji wa haki.
Post a Comment