SERIKALI imezindua mashine mpya tatu za ukaguzi wa mizigo bandarini
zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 20.2 zinazotarajiwa kuongeza mapato
sanjari na kudhibiti dawa za kulevya, usafirishaji wa wanyamapori na
pembe za ndovu.
Akizindua mashine hizo jana katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari
Tanzania (TPA) Dar es Salaam, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
Profesa Makame Mbarawa alisema mashine mbili zitakuwa kwa ajili ya
Bandari ya Dar es Salaam na moja itakuwa katika Bandari ya Tanga.
“Mashine hizi zimetolewa kwa msaada wa Serikali ya China...
Tunawashukuru sana hawa wenzetu kwa kuwa wametusaidia kwa mengi na
ushirikiano wao umekuwa ukisaidia pia katika kukuza uchumi wa nchi
yetu,” alisema Profesa Mbarawa.
Alisema pia wamesaidia mafunzo kwa wataalamu wa TPA, Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) na Kamisheni ya Mionzi iliyopo Arusha ambao ndiyo
watakuwa wasimamizi wa mashine hizo.
“Nasisitiza tuwe waadilifu katika kazi kwa sababu bila uadilifu mashine
hizo zinaweza zisitusaidie... mtu unaweza ukawa na mashine hizi lakini
ukaachia makontena yakapita bila kukaguliwa, hivyo uadilifu na uzalendo
ndivyo vitakavyotusaidia,” alibainisha waziri huyo.
Alisema katika uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, uadilifu ndiyo
jambo kubwa hivyo watahakikisha wanazisimamia mashine hizo ili zifanye
kazi kwa tija na zikitumika ipasavyo, nchi itaweza kupiga hatua kubwa
katika ukusanyaji wa mapato, itawezesha kupambana na dawa za kulevya na
usafirishaji wa wanyamapori.
Aidha, alisema serikali ipo katika utaratibu wa kuagiza mashine nyingine
sita ili kuhakikisha kila bandari inakuwa na mashine hizo na kuongeza
mapato na kuchangia uchumi wa nchi.
Alitoa mwito kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuhakikisha mashine hizo
zinatunzwa vizuri na kufanyiwa matengenezo yanapohitajika kabla
hazijaharibika.
Mapema Balozi wa China nchini, Dk Lu Youqing alisema Bandari ya Dar es
Salaam imetoa mchango mkubwa kwa uchumi wa maendeleo katika nchi nyingi
za Afrika na inategemewa kufanya mapinduzi makubwa ya kiuchumi kutokana
na maboresho yanayofanyika.
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko aliahidi watazisimamia mashine
hizo ili zifanye kazi kwa malengo yaliyokusudiwa na kuongeza ufanisi wa
Bandari.
Post a Comment