Bila shaka, mmoja wa ' Wana- CCM' wa zamani waliofuatilia kwa karibu sana Mkutano Mkuu wa CCM leo ni Fredrick Tluway Sumaye.
Huyu ni mmoja wa wanasiasa walioshindwa sana kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
Ni heri ya Lowassa na Kingunge kulikoni Sumaye. Nilibaki nikimshangaa Sumaye aliposimama majukwaani na kuiponda CCM huku akilaumu pia Katiba inayovikandamiza vyama pinzani.
Katika uchaguzi wa mwaka jana yumkini wapiga kura waliwaadhibu watu wa aina ya Sumaye na kuwaonyesha, kuwa wao wapiga kura si wajinga.
Nilimshangaa Sumaye na Kingunge kusimama majukwaani na kulaumu mfumo ambao wao walishiriki kuujenga na kuulinda. Kwa Sumaye na Kingunge wanapolaumu Tume ya Uchaguzi na Katiba ya Nchi ya mwaka 1977 wanasahau, kuwa wao wakiwa madarakani walikuwa na nafasi ya kuweka mazingira ya kufanyiwa mabadiliko.
Ona Fredrick Sumaye, ukiacha mapendekezo ya Jaji Francis Nyalali ya mwaka 1992 ambayo yaliainisha sheria 40 kandamizi, na hata Sumaye alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu mwaka 1995, sheria hizo 40 kandamizi alizikuta, hakufanya lolote.
Mwaka 1998, Ben Mkapa aliunda Tume ya Jaji Kissanga iliyomkuta Sumaye akiwa Waziri Mkuu. White Paper ile ya Jaji Kissanga, mbali ya mambo mengine, ilipendekeza pia Rais achaguliwe kwa kupata 50 plus asilimia za kura zote.
Ikaenda mbali kupendekeza pia Serikali tatu katika muundo wa Muungano. Nakumbuka pale Diamond Jubilee Hall, Ben Mkapa akiongea na wazee wa darisalaam aliinanga ripoti ya Jaji Kissanga akidai pia haikufuata adidu za rejea. Sumaye alikuwepo kama Waziri Mkuu, alikuwa na nafasi ya kuweka mazingira ya kurekebishwa kwa sheria hizo, lakini, wakati huo, alikaa kimya.
Sumaye alikuwa bize akichimba kisima ambacho leo ameingia mwenyewe.
Niwe mkweli kwa nchi yangu, Fredrick Sumaye wa leo, kama alitaka mabadiliko ya kweli, alipaswa kuendelea kubaki CCM na kuifanya kazi hiyo ndani ya CCM- kama ' Born Again Sumaye' . Si nje ya CCM kama anavyofanya sasa.
Maana, Sumaye angelikuwa na jukwaa pana zaidi na angeaminika zaidi. Nitakuwa mtu wa mwisho kushangaa, pale Sumaye atakapoyashindwa hata maisha ya kila siku ya kisiasa, uko aliko sasa.
Ni mtazamo wangu.
Maggid,
Iringa.
Post a Comment