0
Wafanyakazi wa shirika kubwa la ujenzi la Binladin wameteketeza mabasi kadhaa katika mji mtakatifu wa Makka.

Katika video iliyorushwa kupitia tovuti ya Youtube, wafanyakazi waliokuwa na hasira wa shirika hilo walionekana wakiteketeza mabasi kulalamikia kutolipwa mshahara kwa muda wa miezi mitano sasa.
Ripoti zinasema maandamano ya kupinga hali hiyo hufanyika karibu kila siku nje ya makao makuu ya shirika hilo.

Maandamano hayo yanajiri baada ya shirika hilo kufuta kazi asilimia 25 ya wafanyakazi wake huku Saudi Arabia ikizidi kutumbukia katika mgogoro mkubwa wa kifedha kutokana na kushuka kwa kiasi kikubwa bei ya mafuta ghafi ya petroli katika soko la kmataifa. Siku ya Ijumaa shirika hilo lilitangaza kubatilisha mikataba na wafanyakazi 50,000 wa kigeni.

Shirika la Binladin linasimamiwa na familia maarufu ya Bin Laden ambayo ina uhusiano wa karibu na ukoo wa Aal Saud unaotawala Saudi Arabia. Shirika la Binladin ni la pili kwa ukubwa katika sekta ya ujenzi duniani baada la lile la Vinci Construction la Ufaransa.

Shirika la Binladin lenye makao yake makuu mjini Jeddah lilianzishwa mwaka 1931 na Sheikh Mohammed bin Laden, baba yake kinara wa mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda Osama bin Laden ambaye aliuawa mwaka 2011. Inadaiwa kuwa Osama bin Laden alikanwa na kutengwa na familia yake muongo wa 90.
Kwa mujibu wa tovuti ya Shirika la Binladin, shirika hilo limetekeleza miradi kadhaa muhimu nchini Saudi Arabia kama vile jengo la al-Faisaliah mjini Riyadh, Kituo cha Kifedha cha Mfalme Abdullah, vyuo vikuu kadhaa na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mfalme Abdul Azizi mjini Jeddah.

Post a Comment

 
Top