0
 
 
 
CC
TIMU za soka za Yanga na Azam FC, leo zinakabiliwa na kibarua kigumu zitakaposhuka katika viwanja tofauti kusaka pointi tatu muhimu zitakazosaidia kuongeza kasi kwenye mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo, watakuwa wenyeji wa Mwadui FC katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, huku Azam wakikaribishwa na Mtibwa Sugar Uwanja wa Manungu, Morogoro katika mechi za viporo Ligi Kuu.
Wanajangwani hao waliojikusanyia pointi 53 na kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi wakiwa wamecheza michezo 22, wanawafukuzia mahasimu wao Simba wanaoongoza kwa pointi 57 huku Azam wakiwa nafasi ya tatu kutokana na pointi 52 walizovuna baada ya kushuka dimbani mara 23.
Kwa upande wao Yanga watashuka dimbani wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kipigo cha mabao 3-1, walichotoa dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo uliopita, lakini pia wakisaka ushindi ambao utawaongezea kasi ili kutetea taji la ubingwa.
Akizungumzia mchezo huo kocha wa Mwadui, Jamhuri Kiwhelu ‘Julio’, alisema watahakikisha wanapata ushindi ugenini ili kujiweka katika mazingira mazuri kwenye msimamo wa ligi.
“Mchezo utakuwa mgumu, lakini naamini maandalizi tuliyofanya hatuwezi kushindwa kuondoka na pointi tatu ugenini,” alisema.
Mwadui ambao walilazimishwa sare ya mabao 2-2 nyumbani na Yanga walipokutana kwenye mzunguko wa kwanza, watarudiana na wapinzani wao hao wakiwa na machungu ya kufungwa mabao 2-1 dhidi ya Ndanda FC katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
‘Wanalambalamba’ Azam waliolazimishwa sare katika mechi mbili mfululizo dhidi ya Toto Africans na Ndanda FC, wataingia uwanjani kuikabili Mtibwa huku wakiwa wamepania ushindi ambao utawarudisha kwenye kinyang’anyiro cha kuwania ubingwa msimu huu.
Hata hivyo, Azam watavaana na Mtibwa ikiwa ni siku chache baada ya kutoa kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya timu ngumu ya Esperance ya Tunisia, katika mchezo wa awali wa hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Mtibwa inayoshika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi kwa kujikusanyia pointi 42, itaingia uwanjani ikiwa imepania kulipiza kisasi cha kufungwa bao 1-0 na Azam walipokutana katika Uwanja wa Azam Complex mzunguko wa kwanza.

Post a Comment

 
Top