Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, huenda
akawa Waziri wa kwanza kuliaga Baraza la Mawaziri la Rais wa tano, John
Magufuli, baada ya watu kuanza kuhoji kashfa yake ya kughushi umri wake
ili awanie uenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).
Kashfa hiyo ilibuliwa na wanachama wenzake mwaka 2010 wakati akiwa
Mwenyekiti wa UVCCM, Taifa, na mwishowe ilimng’oa baada ya kuthibitika
kuwa ni kweli alidanganya umri wake ili apate sifa ya kuwania kiti
hicho.
Katika mjadala ulioibuka hivi karibuni kwenye mitandao ya kijamii,
baadhi ya watu wanahoji iweje Rais Magufuli amteue kushika nafasi ya
umma mtu ambaye aliwahi kuthibitika kughushi umri wake kwa maslahi
binafsi.
“Yeye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Wizara ambayo inahusika
moja kwa moja na kukamata na kuwachukulia hatua za kisheria wahalifu,
wakiwemo watu walioghushi nyaraka, sasa kama yeye aliwahi kughushi
kwanini apewe nafasi ya umma,” alihoji mmoja wa wachangiaji wa mjadala
huo kwenye mtandao mmoja wa kijamii na kuongeza:
“Haya mambo ndiyo ambayo baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere alikuwa akiyakataa.
"Inafahamika fika kwamba mtu ana kashfa halafu anapewa nafasi ya uongozi? Watu watajifunza nini kwa mtu
Masauni alidanganya umri wake ili apate nafasi ya kuwania uenyekiti
wa UVCCM mwaka 2008 kutokana na umri wake halisi wakati huo kumnyima
fursa ya kuwania nafasi hiyo.
Kwa mujibu wa Katiba ya UVCCM wakati huo, mtu anayeshika nafasi ya
Mwenyekiti alipaswa kumaliza muhula wake wa miaka mitano kabla ya kuvuka
miaka 35, lakini wakati huo Masauni alikuwa tayari na miaka hiyo hivyo
kukosa sifa za kuwania nafasi hiyo.
Iwapo Masauni angemaliza muhula wake wa miaka mitano bila kusakamwa
na hatimaye kujiuzulu, angeachia nafasi hiyo mwaka 2012 akiwa na miaka
39 umri ambao unakinzana na Katiba ya UVCCM inayopendekeza Mwenyekiti
astaafu akiwa chini ya miaka 35.
Naibu Waziri huyo alifanikiwa kughushi kuonyesha kuwa alizaliwa
Oktoba 3, 1979 ingawa baba yake mzazi alipohojiwa alikana mwaka huo
uliotajwa na mwanaye kwenye nyaraka zake na kusema alizaliwa Oktoba 3,
1973.
Baada ya Masauni kufanikiwa kughushi umri wake watu walianza
kufuatilia historia yake na kubaini kuwa alianza shule ya msingi mwaka
1979 hivyo kuhoji iweje mtoto azaliwe mwaka huo huo na aanze shule ya
msingi wakati huo huo.
Mjadala huo ulikuwa mkali kiasi cha kusababisha watu kumtafuta baba
yake mzazi ambaye alikiri kuwa mtoto wake huyo alighushi umri wake
kwasababu hakuzaliwa mwaka huo alioutaja kwenye nyaraka zake za kuombea
hati ya
Baada ya kuthibitika kwamba umri uliotajwa na Masauni si halisi,
Naibu Waziri huyo alianza kuandamwa na hatimaye aliamua kujizulu mbele
ya Baraza Kuu la UVCCM lililoketi mkoani Iringa mapema 2010.
Vuguvugu la kumng’oa Masauni lilianza mapema na mpango huo ulisukwa
vyema na waliokuwa wakiimezea mate nafasi hiyo hivyo mara tu kikao
hicho kilipoanza kwenye ukumbi wa Siasa ni Kilimo, Masauni alianza
kushambuliwa kuhusu shutuma zinazomkabali na hatimaye kuamua kubwaba
manyanga.
Baadhi ya wajumbe walisema hawako tayari kuingia katika kikao hicho
kama ajenda ya kumjadili Mwenyekiti Masauni haitakuwepo na ajenda hiyo
ilipowasilishwa tu Masauni hakuwa na chaguo zaidi ya kung’oka.
Lakini tangu ithibitike kuwa ameghushi umri wake, hakuna hatua
zozote za kisheria alizochukuliwa na wala hajawahi kufikishwa mahakamani
jambo ambalo lilianza kuzua maswali kama kuna watu wako juu ya sheria.
Hatua ya Rais Magufuli kumjumuisha kwenye Baraza la Mawaziri
kumeelezwa kwamba ni sawa makosa kwani mtu aliyewahi kuthibitika kuwa
ameghushi cheti hawezi kuwa na sifa ya kuteuliwa kuongoza ofisi ya umma.
Rais mstaafu Jakaya Kikwete alithibitisha Masauni kudanganya umri akiwa Mwenyekiti wa CCM Mei, 2010.
Kikwete alikaririwa akisema Masauni hakuonewa wala kufanyiwa fitina
bali alijiuzulu kutokana na kudanganya kuhusu umri wakati wa mchakato
wa Uchaguzi Mkuu wa Jumuiya hiyo 2008.
Kikwete alisema kuwa Masauni alitamka kuwa alizaliwa mwaka 1979 wakati uchunguzi ulibaini kuwa alizaliwa Oktoba, 1973.
Kikwete aliyasema hayo baada ya kufungua kambi ya wiki moja ya
UVCCM kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2010 katika
Kijiji cha Ihemi, wilayani Iringa Vijijini, Mkoa wa Iringa, ambapo
aliongeza kuwa Masauni hakuwa mkweli na kwamba uamuzi wake wa kujiuzulu
usingeepukika.
Alisema kuwa suala la umri sio tukio la kwanza katika UVCCM kwa
kuwa kuna baadhi ya wanachama wake waliozuiwa kugombea nafasi fulani za
uongozi kutokana na kuzidi umri.
Mwenyekiti huyo wa CCM alisema: ”Hakuna uchawi, ni kanuni na ni lazima kusimamia sheria na kanuni, hatutafumba macho.”
Kabla ya uchaguzi wa UVCCM 2008 kulitokea mvutano wa makundi
yaliyokuwa yanataka kusimika watu wao kwenye nafasi ya Mwenyekiti, hasa
kutoka Bara.
Mvutano huo ndio ulimlazimu Mwenyekiti wa Chama, Kikwete wakati
ule kuamua kiongozi wa UVCCM apatikane kutoka Zanzibar ili kutuliza hali
ile ya makundi, hali iliyomuibua Masauni kuwa Mwenyekiti.
Gazeti hili lilifanya jitihada za kuzungumza na Masauni mwenyewe na
mkuu wake wa karibu, Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga, lakini
jitihada hizo hazikuzaa matunda baada ya simu zao kuita muda mwingi
bila kupokelewa.
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa naye
alipotafutwa atoe ufafanuzi wa madai ya watu kwamba Rais Magufuli
amemteua mtu mwenye kashfa, simu yake ya mkononi iliita muda mrefu bila
kupokelewa jana Jumamosi.
Post a Comment