0

                Rais Magufuli
Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Marekani la Changamoto za Milenia (MCC), imiesitisha rasmi mkataba wa awamu ya pili ya kutoa msaada wa Dola milioni 472 sawa na Shilingi trillion moja, kwa Tanzania kwa maelezo kwamba ,haijaweka sawa masuala ya kidemokrasia.

Madai ya MCC shirika linalohusika kusaidia nchi zinazoendelea lililoundwa na Bunge la Marekani, mwaka 2004, baadhi ya vigezo vinavyotumiwa kutoa misaada ni pamoja na kuangalia mafanikio katika mambo makubwa ambayo ni uongozi wa haki, kuwekeza kwa wananchi na kupanua uhuru wa kiuchumi.

Itakumbukwa kuwa kabla ya kuchukua hatua hiyo, mwaka 2015, MCC ilitoa Dola milioni 698 karibu Shilingi trilioni 1.46, zilizowekezwa katika miradi mbalimbali ya maendeleo.

Sababu zinazotajwa ni pamoja na kutoridhishwa na kitendo cha kurudia uchaguzi wa rais, wawakilishi na madiwani visiwani Zanzibar bila ya kushirikisha pande zote. Pili utekelezaji wa sheria ya makosa ya mtandao kuhusu uhuru wa kujieleza.

Baadhi ya wanasiasa wameanza kuibebesha lawama serikali ya Rais John Magufuli , wakidai imesababisha misaada hiyo kusitishwa kwa vile ilikataa kujihusisha na marudio ya uchaguzi wa Zanzibar.

Siyo dhambi kwa serikali ya sasa kunyooshewa kidole kwa madai kwamba haikushughulikia suala la uchaguzi wa marudio ya uchaguzi Zanzibar; hata hivyo sababu walizotoa MCC hazikuwa na mashiko. Nasema hivyo kwasababu marudio ya uchaguzi yalitangazwa mapema lakini MCC hawakujitokeza wazi wazi kupinga hatua hiyo ya kurudiwa kwa uchaguzi. sheria ilifuatwa kama ilivyoainishwa kwenye katiba ya Zanzibar.

Kama hiyo haitoshi, wapinzani wenyewe ndiyo waliokataa kushiriki kwenye uchaguzi huo wa marudio. Wahenga walinena; “unaweza ukampeleka ng’ombe mtoni lakini huwezi kumshurutisha kunywa maji” serikali ya Magufuli haikuwa na uwezo wa kuwashurutisha wapinzani kuingia kwenye uchaguzi.

Aidha, haiwezi kubebeshwa lawama kwasababu mambo hayo yalitokea katika serikali ya awamu ya nne chini ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete. Muda ulikuwa mfupi kwa Rais Mafuli kusoma alama za nyakati.
Pamoja na yote hayo, lazima tukubaliane kwamba kasi aliyoingia nayo Rais Magufuli ya kutaka kuimarisha uchumi wa ndani na kufuta dhana ya utegemezi, haijawafurahisha mataifa mengi ya Magharibi ikiwamo na Marekani.

Mataifa hayo yalizoea kuwachukulia kiwepesi marais wapya wa Afrika kama vitoto vya ndege vinavyosubiri kwenye viota majaliwa ya mama kuviletea wadudu na kuwalisha. Viongozi wengi wa Kiafrika walijenga desturi na utamaduni wa kukimbilia nchi hizi kupitisha bakuli za misaada jambo ambalo halikutokea kwa Rais Magufuli.

Sambamba na hilo, mataifa mengi ya Magharibi yanaishangaa Tanzania kuendelea kuimarisha amani na utulivu hata baada ya rais mpya kuingia madarakani. Hivyo MCC wanataka kudhoofisha nguvu za Rais Magufuli?

Mazingira kama haya yanatosha kuonyesha kwamba, mataifa makubwa yanatamani kuona Bara la Afrika likiendelea kutawaliwa kupitia mlango wa nyuma wa ukoloni mamboleo na utandawazi kwa maana ya misaada yenye masharti magumu.

Tukirejea kauli ya mgombea mtarajiwa wa urais wa Marekani kupitia chama cha Republican Donald Trump alitoa kauli katika moja ya kampeni zake kuwa bara hili linahitaji tena kukandamizwa. Akisema :“Afrika mambo yake ni bado sana na ili kuiweka sawa inatakiwa itawaliwe na wakoloni kama mwanzo kabla ya kujitawala wenyewe au ikombolewe upya”
Si hayo tu aliwahi kusema Waafrika hawafai kwa lolote ni wezi, wavivu , wasiofikiria na kwamba wanachoweza kujamiiana!

Kauli ya Trump ni kielelezo kinachowakilisha mtizamo wa viongozi wengi wa Magharibi na wakiwamo baadhi ya wajumbe wa Bodi ya MCC. Vijisababu vilivyotolewa havimshawishi mtu kuamini kuwa Marekani na marafiki zake hawakutarajia kuona ujasiri huu wa Rais katika kupangua desturi iliyozoeleka ya Afrika ambayo wanatamani iendelee kubaki “black continent”.

Tanzania imekuwa ikisifika nje na kutolewa mfano kuwa miongoni mwa nchi zilizopiga hatua kubwa katika kutekeleza Azimio ya Umoja wa Mataifa (UN) kususan katika kuheshimu haki za binadamu na uhuru wa kujiendeleza.

Niseme tu kwamba fedha ni zao, uamuzi ni wao na pia hatuwezi kuwapangia walichokiamua ila tusiruhusu kazi nzuri aliyoianza Rais Magufuli itiwe doa na hao wenye fikra mgando wasiopenda kuiona Afrika ikipiga hatua moja mbele kufuta dhana ya utegemezi.

Heri tukose misaada hizo lakini tubaki na uhuru wa kuamua mambo yetu wenyewe. Hakuna jambo lisilokuwa na mwisho hata hiyo bodi ya MCC haitadumu milele. Serikali ya Rais Magufuli haistahili kubebeshwa lawama.
Mawasiliano: 0713 399 004, 0767 399 004,jmkibasso@gmail.com
 

Post a Comment

 
Top