0

                    Rais wa TFF, Jamal Malinzi.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi, amesema "wamechanganyikiwa" baada ya Serikali kuzishikilia baadhi ya mali za shirikisho hilo la soka nchini, huku akihofu kutaifishwa kwa Uwanja wa Karume.

Baada ya kuzifunga akaunti zote za TFF na kuchukua pesa zote zilizokuwamo kiasi cha Sh. milioni 250, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jana ilirejea tena Karume zilipo kwenye ofisi za shirikisho hilo na safari hii ikiondoka na magari matano kutokana na kulidai kitita kikubwa cha fedha.

Shirikisho hilo lenye mamlaka ya juu ya soka nchini, linadaiwa Sh. bilioni 1.6 ambazo zinatokana na ukwepaji kodi katika mishahara ya makocha wa timu za taifa (Jan Poulsen na Kim Poulsen) pamoja na kutokatwa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika mapato ya mechi ya Taifa Stars dhidi ya Brazil iliyoingiza Sh. bilioni 1.8.

Richard Kayombo, Mkurugenzi wa Elimu na Huduma kwa Walipakodi wa TRA, jana alithibitisha mamlaka hiyo kushikilia magari hayo ya TFF ili shirikisho hilo lilipe deni la malimbikizo ya kodi mbalimbali.

"Ni kweli tumekamata magari matano ya TFF," alisema. "Mpaka sasa tunawadai shilingi bilioni 1.118 ambayo ni kodi mchanganyiko kuanzia mwaka 2010 hadi 2015.

"Kodi hizo ni VAT, 'Paye' na SDL, ikumbukwe hapo nyuma tulikamata akaunti zao tulipokuwa tukiwadai Sh. bilioni 1.6 na tukapunguza sehemu ya deni, lakini bado halijaisha na ndiyo sababu ya kukamata hayo magari matano."

Kwa mujibu wa Kayombo, magari hayo yapo kwenye moja ya vituo vitio vya magari (yard) vya jiji la Dar es Salaam, basi kubwa la Taifa Stars likiwa ni mojawapo.

Akizungumzia uamuzi huo wa TRA katika mkutano na waandishi wa habari jijini jana mchana, Malinzi alisema: "Tumechanganyikiwa, ni sawa na familia yenye msiba, unailetea taarifa nyingine mbaya."

"Tumepata hasara kubwa (Sh. milioni 250) kutokana na kujitoa kwa Chad kushiriki michuano ya Afrika mwaka huu, tunaongezwa tatizo jingine."

Malinzi alidai Wizara yenye dhamana ya michezo ndiyo inapaswa kutupiwa lawama kwa kutolipa kodi ya mishahara ya makocha.
'Kigogo' huyo wa TFF alisema magari yaliyokamatwa hayana thamani ya pesa wanayodaiwa hivyo, "Watanzania wasishangae watakaposikia Uwanja wa Karume (unaomilikiwa na TFF) umetaifishwa."
 

Post a Comment

 
Top