0

RAIS wa Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Peter Chisawilo ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuondoa tozo zisizo za lazima kwenye mamlaka za udhibiti ambazo zimekuwa kero inayowaongezea gharama za uendeshaji.

Chisawilo alitoa ombi hilo wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa chama hicho mkoa wa Tanga.

Alisema ili kukiwezesha chama kuendelea kutekeleza majukumu na shughuli zake mbalimbali kwa uhuru, ni vema serikali ikawaondolea utitiri wa tozo ambazo zimekuwa zikilipwa sasa na mamlaka za udhibiti, hatua inayoongeza gharama za uendeshaji.

“Lengo la serikali la kuunda mamlaka na bodi za usimamizi ni kuweka utaratibu mzuri wa usimamizi na utendaji, lakini kwa sasa mamlaka hizo zimegeuza tozo kama chanzo chake cha mapato hali ambayo inawaongezea wafanyabiashara mzigo wa gharama”, alisema.

Akizungumzia fursa za biashara na uzalishaji, Chisawilo aliwataka wafanyabiashara pamoja na wamiliki wa viwanda kuhakikisha wanajiamini.

“Katika suala hili hakuna ubishi kwamba ninyi wafanyabiashara na wenye viwanda lazima mjiamini kwa kuihakikishia jamii pamoja na washindani wenu sokoni kwamba mnao uwezo wa kuzalisha bidhaa bora. Nawahimiza msiishie hapo tu, kaingieni mikataba mikubwa mfano katika mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta linalotarajiwa kujengwa kutoka Uganda hadi Tanga”, alisema.

Awali Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Tanga, Paul Bwoki akisoma taarifa ya utendaji, alisema wanachama hawana budi kuongeza ubunifu ili wanufaike na rasilimali za asili zilizopo mkoani hapa.
Katika mkutano huo ambao walichagua pia viongozi, Deo Ruhinda alichaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa TCCIA kwa mkoa ambapo nafasi ya makamu mwenyekiti upande wa kilimo ilichukuliwa na Juvent Magogo.

Oswin Hosea amekuwa makamu mwenyekiti upande wa viwanda pamoja na Daudi Mwai aliyechaguliwa kuwa mweka hazina.

Post a Comment

 
Top