UONGOZI wa klabu ya Stand United ya Shinyanga umesema hauna mpango wa kumuweka kitimoto Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mfaransa Patrick Liewig, kutokana na uamuzi wake wa kuwaweka benchi wachezaji wakongwe na wazoefu katika kikosi hicho.
Awali ilidaiwa kuwa kocha huyo atawekwa kitimoto na uongozi wa klabu hiyo ili aweze kutoa sababu za kutowachezesha wachezaji wazoefu katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara, akiwemo Elius Maguli na kuifanya timu hiyo kupata matokeo yasiyoridhisha.
Stand inashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi kwa kujikusanyia pointi 31, baada ya kushuka dimbani mara 24, ambapo kesho wanatarajia kukutana na Mgambo Shooting katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Chanzo cha habari za ndani ambazo zimelifikia MTANZANIA jana, kimedai kuwa uongozi wa klabu hiyo umeelezea kukubaliana na kuheshimu uamuzi uliofanywa na kocha huyo.
“Liewig ni kocha mkuu, hivyo uamuzi wake katika benchi la ufundi ni lazima uheshimike ndani ya klabu, kwani hata ukiangalia timu haipo katika nafasi mbaya kwenye msimamo wa ligi.
Chanzo hicho kilidai kuwa si lazima kila mchezaji aliyesajiliwa ndani ya timu hiyo acheze, kwani wanaopangwa kucheza katika kikosi wanapimwa kulingana na ubora wa viwango vyao na uwezo walionao uwanjani.
“Kocha ndiye mwenye nafasi ya kujua mchezaji anayefaa, hivyo wachezaji wanatakiwa kujituma uwanjani ili waweze kumshawishi wakati wa kupanga kikosi kitakachosaidia kupatikana kwa matokeo ya ushindi,” kilieleza chanzo hicho.
Post a Comment