Mshukiwa wa mauaji
ya kimbari nchini Rwanda Ladislas Ntaganzwa amefikishwa kwa mara ya
kwanza mbele ya mahakama mjini Kigali wiki mbili baada ya kukabidhiwa
Rwanda toka Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Anashtakiwa kuhusika katika mauaji ya kimbari na ubakaji alipokuwa mkuu wa wilaya ya Nyakizu kusini mwa Rwanda mwaka 1994.
Bw Ntaganzwa amefikishwa mahakamani chini ya ulinzi mkali wa askari polisi pia kukiwa na watu wengi waliokuja kuhudhuria kesi wakiwa ni manusura wa mauaji ya kimbari kutoka wilaya ya Nyakizu.
Mwendesha mashtaka amemfunguliwa mashtaka matano yakiwemo mauaji ya kimbari, kuhamasisha genge la Wahutu kutekeleza mauaji hayo na ubakaji.
Ameiambia mahakama kuwa mtuhumiwa alitekeleza makosa hayo katika sehemu mbali mbali za wilaya ya Nyakizu, kusini mwa Rwanda.
Alipoulizwa kuhusu hoja ya mwendesha mashtaka, mshtakiwa ameamua kukaa kimya na hakutoa jibu lolote.
Wakili wake amesema kuwa hana lolote ya kuiambia mahakama hii ya mwanzo akisisitiza haina mamlaka ya kuendesha kesi hiyo.
Mwandishi wa BBC Yves Bucyana anasema kesi dhidi ya Bw Ntaganzwa, sawa na za watuhumiwa wengine wa mauaji ya kimbari waliokuwa wanasakwa na mahakama ya kimataifa kwa ajili ya Rwanda ICTR, inasikizwa na kitengo maalumu cha mahakama kuu nchini Rwanda baada ya kufungwa kwa ICTR mwishoni mwa mwaka jana.
Jaji alisema kesi ilioanza leo ni ya mwanzo na kusudi lake ni kutafuta kifungo cha muda kabla ya kesi yenyewe kuanza kusikilizwa kwa undani wake.
Bw Ntaganzwa
Post a Comment