0

                  Hii ni mara ya pili kwa Rais Magufuli kufuta sherehe za sikukuu
Rais wa Tanzania John Magufuli ameahirisha sherehe za maadhimisho ya Siku ya Muungano na badala yake akawataka Watanzania waiadhimishe wakiwa majumbani au wakiwa katika shughuli zao binafsi.

Siku hiyo hata hivyo bado itasalia kuwa ya mapumziko kama kawaida. Agizo hilo la Dkt Magufuli aidha linaathiri shamrashamra za mwaka huu pekee.

Siku hiyo huadhimishwa tarehe 26 Aprili kila mwaka kukumbuka siku sawa na hiyo mwaka 1964 ambapo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliundwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar (inayojumuisha Visiwa vya Pemba na Unguja).

Dkt Magufuli amesema fedha ambazo zilipangwa kutumika kwa ajili ya kugharimia vinywaji, vyakula, gwaride, halaiki, burudani mbalimbali na hafla ya usiku ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni mbili za Tanzania zitumike kupanua barabara ya Mwanza Airport katika eneo linaloanzia Ghana Quarters hadi uwanja wa ndege wa Mwanza.

Barabara hiyo inafanyiwa upanuzi kutatua msongamano wa mkubwa wa magari ambayo umekuwa ukiathiri shughuli eneo hilo.
Dkt Magufuli amekuwa mapumzikoni nyumbani kwake eneo la Chato, kaskazini magharibi mwa Tanzania.

Post a Comment

 
Top