0


machinga
AGIZO la Mkurugenzi wa Halmashauri  ya Manispaa  ya Morogoro, Theresia Mahongo kupiga marufuku wafanyabiashara wa Soko la Mitumba la Sabasaba,  jana liligonga mwamba   baada  ya  wafanyabiashara  hao kuwagomea askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU).

MTANZANIA  liliwashuhudia  wafanyabaishara  hao wakiendelea kupanga biashara  zao  barabarani bila kujali askari  na mgambo wa manispaa waliokuwa wamevalia sare zao.

Askari hao walipoona hali hiyo, waliamua  kuondoka baada  ya  wafanyabiashara  hao  kuanza  kujikusanya   kutaka kuvamia gari  la  manispaa  lililokuwa limebeba FFU  na mgambo.

Wakizungumzia hali hiyo, baadhi ya wafanyabiashara walisema waliamua kuwagomea askari hao kutokana uongozi huo  wa manispaa  kuwazuia kufanyabiashara  kando kando  ya  barabara huku ikiwaruhusu baadhi yao.

“Tunashangazwa na uongozi kutuzuia sisi  huku Sabasaba, lakini wanaacha  wafanyabiashara kule mjini eneo la Islam ambako  ni mjini kabisa,“ alisema Jalala Uweso, mmoja  wa wafanyabiashara wa mitumba.

Hata  hivyo,  wafanyabiashara  hao wameiomba manispaa  kuwaandalia  eneo  lenye  miundombinu muhimu  na inayofikiwa na wateja kwa urahisi kabla ya kuwafukuza  katika eneo hilo ambalo lina wateja wa kutosha.

Post a Comment

 
Top