-
- “MIAKA ya nyuma kabla hatujapata elimu ya usafi wa mazingira wengi walikuwa hawana vyoo na walikuwa wakijisaidia vichakani au porini”.
Ni maneno ya Julieta Saileni, mkazi wa Ugogoni Kongwa Mjini, mkoani
Dodoma. Mwananchi huyo anasema, wakati huo ustaarabu wa kujisaidia
chooni haukuwepo na kwamba, watu walikuwa wakijenga nyumba zisizo na
vyoo. Julieta anasema sasa hali imebadilika, hakuna vyoo vya magunia
eneo hilo. Kwa mujibu wa mwananchi huyo, mazoea ya kujisaidia vichakani
na wakati mwingine karibu na vyanzo vya maji hayapo tena. Anasem
a kaya
nyingi zina vyoo vilivyoboreshwa na vinavyotumika.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Ugogoni Sarah Kimonga anasema, kabla ya
kutolewa kwa elimu chini ya Mradi wa Usafi wa Mazingira Tanzania (UMATA)
kaya zilikuwa zikishirikiana vyoo kwa kuwa ujenzi wa vyoo haikuonekana
kama ni jambo muhimu.
“Hali hiyo ilisababisha kinyesi kutapakaa kila mahali hasa porini.
Tulikuwa tukiogopa hata kutembea kwenye majani,” anasema Kimonga.
Anasema watu sasa wamestaarabika na mlipuko wa magonjwa haupo tena.
Ofisa Afya Kata ya Ugogoni, Iqubal Janja anasema, wakati wa kampeni hiyo
ikianza asilimia 80 ya wananchi hawakuwa na vyoo lakini kutokana na
uhamasishaji watu wamebadilika na kuona umuhimu wa kaya kuwa na choo
bora na kukitumia.
“Wengi walikuwa wakiishi kwa mazoea kwani alikuta mzazi wake akiwa
hana choo na hivyo waliona hakuna umuhimu wa kuwa na choo,” anasema
Janja. Mtendaji wa kijiji cha Ugogoni, Cecilia Bajuta anasema hali
ilikuwa mbaya kwa kuwa wananchi wengi hawakuwa na vyoo na walipelekwa
kwenye Baraza la Migogoro la Kata. Anasema, wananchi hao walilazimishwa
kujenga vyoo na aliyeshindwa alilipa faini Sh 50,000 na kusimamiwa hadi
alipokijenga.
Anasema jumla ya wananchi 13 tayari wamefikishwa katika baraza la
migogoro na kuchukuliwa hatua na wote sasa wana vyoo. Mkuu wa Wilaya ya
Kongwa, Bituni Msangi anasema kampeni ya UMATA ni ya kitaifa na
inatekelezwa katika wilaya zote Tanzania.
“Wilaya yetu ya Kongwa ni moja kati ya wilaya tatu za mkoa wa Dodoma
zikiwemo wilaya nyingine za Bahi na Chamwino zinazosimamiwa na shirika
la kimataifa la Plan pamoja na mashirika mengine ya utekelezaji likiwemo
SAWA ambao wamekuwa wakishirikiana nasi kuanzia ngazi ya wilaya, kata,
vijiji na vitongojini katika kuhamasisha masuala ya afya na usafi wa
mazingira,” anasema Msangi.
Mfuko wa Usafi wa Mazingira Duniani (GSF) umeona ni muhimu kusaidia
jamii kuondokana na maradhi yatokanayo na ukosefu wa vyoo pamoja na
kutonawa mikono kwa maji na sabuni. Msangi anasema, shirika la SAWA
limekuwa likifanya uhamasishaji huo katika vijiji 23 katika kata saba za
Ugogoni, Sejeli, Songambele, Mkoka, Matongoro, Makawa na Zoissa katika
awamu ya kwanza kuanzia Septemba 2015.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, hadi sasa Kijiji cha Ugogoni chenye
vitongoji vitatu kimekuwa cha kwanza kumaliza kazi ya usafi wa mazingira
hatua ya pili. Anasema, kabla ya mradi, wananchi wengi wa Wilaya ya
Kongwa hawakuwa na vyoo; kwa tafsiri rahisi ni kuwa walikuwa
wanajisaidia kwenye vyoo vya majirani vichakani na porini, hivyo
kuchafua vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla. Uchafu huo
ulisababisha magonjwa ya kuharisha, kipindu pindu na yale yanayotokana
na maji machafu.
“Tunahitaji kuwa na mpango mkakati wa makusudi utakaotuwezesha
kufikia hatua ya kwanza katika kipindi kifupi kijacho,” anasema Msangi.
Anasema, kwa miezi kadhaa sasa Tanzania imekumbwa na ugonjwa wa
kipindupindu. Takribani mikoa 18 imeripotiwa kuathiriwa na ugonjwa huo
na kwamba, katika wilaya hiyo kipindupindu kimeathiri Tarafa ya Zoissa.
Chanzo kikuu cha ugonjwa huo ni kula vyakula vilivyo na vimelea vya
ugonjwa ambavyo hukaa kwenye kinyesi na husambazwa na nzi au kugusa,
kushika kinyesi.
“Wagonjwa wengi wameripotiwa na baadhi ya ndugu zetu, Watanzania
wenzetu wamepoteza maisha,” anasema Msangi. Anasema Serikali inatumia
fedha nyingi kununua dawa na vifaa tiba ili kukabiliana na ugonjwa ambao
wananchi wangeweza kuuzuia kwa kujenga vyoo na kuvitumia, kunawa mikono
kwa sabuni na kutibu maji ya kunywa. “Fedha zinazotumika kutibu
kipindupindu zingeweza kutumika kwenye miradi mingine ya maendeleo. Njia
rahisi ya kuzuia kipindupindu ni kukata mawasiliano ya nzi na kinyesi
au mtu kula kinyesi; hii ni pamoja na kuhakikisha hakuna nzi anayeingia
na kutoka chooni” anasema Msangi.
Anataja njia nyingine ya kumaliza kipindupindu ni kuweka mfuniko
kwenye tundu la choo muda wote, kumiminia dawa au majivu mara kwa mara
ili kuondoa harufu ambayo ingeweza kumvutia nzi. Kusafisha tundu la choo
ni safi, kuondoa mabaki ya kinyesi, na kusafisha eneo lililokuwa na
kinyesi ni namna nyingine ya kukabili ugonjwa huo. Anataka viongozi na
watendaji wa Serikali kila ngazi wamepewa maagizo kuhusu namna ya
kulisimamia hilo na kutaka kila mwananchi awe mstari wa mbele kuitikia
mwito wa kuutokomeza ugonjwa huo.
Msangi akitaka vijiji vingine wilayani huo kuiga yaliyofanywa Ugogoni
ili kuondokana na aibu ya kujisaidia hovyo vichakan. Mmoja wa
wafanyakazi wa Shirika la SAWA, Asnat Charles anasema, katika mradi huo
wa usafi wa mazingira shirika hilo linahamasisha ujenzi na matumizi ya
vyoo bora na mabadiliko ya tabia katika jamii na shuleni.
Anasema, SAWA wanatumia mbinu ya kushirikisha jamii kuhusu usafi wa
mazingira kwa kutumia mbinu iitwayo CLTS (Community Led Total
Sanitation) na miongozo ya taifa ya maji, afya na usafi wa mazingira
katika wilaya ya Kongwa. Mradi huo pia unatoa elimu ya afya na usafi wa
mazingira kwa shule za msingi ikimlenga mtoto ambaye ndiye chachu ya
mabadiliko kwa mtoto mwenzake, ngazi ya familia na jamii kwa ujumla.
Anasema katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi wa UMATA
shirika la SAWA kuanzia mwishoni wa Septemba mwaka 2015 linafanya kazi
katika kata saba za Ugogoni, Sejeli, Songambele, Mkoka, Zoissa,
Matongoro na Makawa “Mpaka sasa tumefanikiwa kufanya uhamasishaji wa
matumizi sahihi ya vyoo, ujenzi wa vyoo na usafi wa mazingira kwa ujumla
kwa kupitia mikutano ya hadhara, kutoa mafunzo ya afya na usafi wa
mazingira kwa wahudumu wa afya 332, viongozi ambao ni watendaji kata
saba vijiji 23, Vitongoji 83, waratibu wa elimu kata saba na walimu 44
katika shule 22 za msingi,” anasema Charles.
Anasema, kutokana na muongozo wa Wizara ya Afya, ili kijiji au
kitongoji kifikie hatua ya pili ya uboreshaji wa masuala ya usafi wa
mazingira inahitajika kuwa na vigezo kikiwemo cha kila kaya kuwa na choo
kinachotumika na kifaa cha kunawa mikono yaani asilimia 100 ya vyoo kwa
jamii na vifaa vya kunawa mikono. Taasisi zilizomo katika jamii
zinapaswa kuwa na vyoo bora na vifaa vya kunawa mikono, na kutokuwepo
kwa dalili za uzagaaji ovyo wa kinyesi katika mazingira yakiwemo
makorongo, karibu na vyanzo vya maji na viwanja vya wazi katika jamii
husika.
Anasema hadi sasa vitongoji vingi vilivyopo chini ya shirika la SAWA
vipo katika hali nzuri ya kuacha kujisaidia ovyo kwani vipo kwenye hatua
zaidi ya asilimia 75 ya utekelezaji wa mradi. “Hii ni hatua nzuri
ukilinganisha na hali ilivyokuwepo mwanzo kabla ya utekelezaji wa mradi.
Hatua hii imechangiwa sana na ufuatiliaji wa mara kwa mara katika ngazi
ya kaya ili kuhakikisha wale watu ambao hawana vyoo wanajenga na pia
kuhimiza umuhimu na faida za kunawa mikono kwa maji yanayotiririka hasa
kwa kutumia teknolojia rahisi ya kibuyu chirizi,” anasema Charles.
Post a Comment