0
                                                      Google imeomba radhi
Google imelazimika kuondoa kitufe cha Siku ya Wajinga kutoka kwenye huduma yake ya barua pepe ya Gmail baada ya watu wengi kulalamika.

Kitufe hicho kilikuwa kinatuma video za mzaha kwa watu walio kwenye anwani ya mtu.

Kitufe hicho kilikuwa kimewekwa karibu na kitufe cha kawaida cha kutuma barua pepe na kiliwawezesha watumizi wa Gmail kusitisha mawasiliano ya kawaida na badala yake kutuma video fupi ya gif ya kibonzo kikiweka chini maikrofoni.

Watu wengi wamelalamika sana kuhusu kitufe hicho kwenye kumbi za Google.

Kuna wanaosema wamefutwa kazi baada ya kuwatumia wakubwa wao barua pepe za mzaha, wengine wanasema wametuma barua pepe za mzaha kwa kampuni ambazo walikuwa wanaomba kazi.

Mwandishi mmoja aliandika kwamba alikuwa anataka kutuma makala zake kwa mhariri na muda ulikuwa unapita akatuma haraka. Alisubiri jibu lakini hakupata. Baadaye aligundua kwamba kimakosa alibofya kitufe cha mzaha.

Kampuni hiyo imeondoa kitufe hicho na kuomba radhi.

"Inaonekana kana kwamba tumejitania sisi wenyewe mwaka huu,” Google imesema kupitia taarifa.
"Kutokana na hitilafu katika utengenezaji wa kitufe hiki, kiungo cha kuweka maikrofoni chini (MicDrop) kilisababisha kilio kuliko kicheko. Tunaomba radhi.”

Google ilitangaza kuanzishwa kwa Gmail tarehe 1 Aprili 2004 na wakati huo wengi walidhani ulikuwa mzaha wa Siku ya Wajinga.

Post a Comment

 
Top